Walioiba nondo ‘flyover’ Ubungo, kulipa fidia Sh30 milioni

Friday January 10 2020

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania imewahukumu watu watatu, akiwamo mmiliki wa kumbi za sherehe za Mrina, Maiko Mrina (67) kulipa fidia ya Sh30 milioni kwa pamoja, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa tani nane za Nondo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba tani nane za nondo za ujenzi wa barabara ya juu eneo la Ubungo, Dar es Salaam linaloendelea kujengwa kwa sasa.

Mbali na kulipa fidia, mahakama hiyo imewahukumu kulipa faini ya Sh3 milioni kila mmoja au kwenda jela miaka saba.

Pia, Mahakama hiyo imeamuru tani nane za nondo walizoiba washtakiwa hao, zirudishwe katika kampuni ya China Civil Engineering Contraction Corporation.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na fidia hiyo na hivyo kuachiwa huru.

Mbali na Mrina, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 140/2019 ni dereva, Ally Athumani (36) mkazi wa Mbagala na mlinzi Shabani Rashidi (57)mkazi wa Mwananyamala.

Advertisement

Washtakiwa hao wametiwa hatiani leo Ijumaa Januari 10,2020 baada ya kukiri mashtaka yao na kumuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) wakiomba wasamehe na wapunguziwe adhabu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo, amesema washtakiwa wametiwa hatiani katika shtaka la wizi.

"Mmetiwa hatiani katika shtaka la wizi, hivyo wote kwa pamoja mnatakiwa kulipa fidia ya Sh30 milioni," amesema hakimu Mwaikambo

"Pia, mahakama hii imewapiga faini ya Sh3 milioni kwa kila mshtakiwa na kama atashindwa kulipa basi atatumikia kifungo cha miaka saba," amesema Hakimu

Hakimu Mwaikambo amesema mbali na fidia na faini hiyo, nondo hizo zinatakiwa zirudishwe katika kampuni ya China Civil Engineering Contraction Corporation.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya akisaidiana na Faraji Nguka, aliomba  mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa Athuman na Rashid,  walifikishwa Kisutu  Desemba 24, 2019 na kusomewa mashtaka matatu, ambayo ni wizi, kuisababishia hasara Serikali na kutakatisha fedha.

Wakati Athuman na Rashid wakisomewa mashtaka yao Mahakamani hapo, Mrina yeye  alisomewa mashtaka yake hospitalini, akiwa amelazwa wodi namba mbili katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dar es Salaam baada ya kuugua.

Katika kesi ya msingi, Athumani pekee, anadaiwa kuwa Agosti 29 na Agosti 30, 2018, eneo la Ubungo, akiwa mwajiliwa wa Kampuni ya China Civil Engineering Contraction Corporation aliiba tani nane za Nondo zenye thamani ya Sh30.40 milioni mali ya kampuni hiyo, zilizofika kwake kutokana na nafasi yake ya ajira.

Pia, kati ya Agosti 29 hadi 30, 2018 katika Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa nia ovu waliisababishia Serikali hasara ya Sh30.40 milioni.

Katika shitaka la tatu inadaiwa kuwa, Agosti 29, 2018, washitakiwa kwa pamoja walitakatisha kiasi hicho cha fedha wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la wizi.

Advertisement