Walioshinda uenyekiti Moshi wafundwa

Wednesday November 27 2019

By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Moshi. Viongozi wapya wa vijiji na vitongoji katika Halmashauri ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kusimama vyema kwenye nafasi zao kuhakikisha wanamsaidia Rais John Magufuli, kutatua kero za wananchi na migogoro katika maeneo yao.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 27, 2019 na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kastory Msigala.

Alikuwa akizungumza nao muda muda mfupi baada ya kula kiapo na amesema vijiji vingi viko katika hali mbaya kutokana na viongozi wake kushindwa kufanya kazi kama nafasi zao zinavyoelekeza.

Amesema bado kuna migogoro mingi kama ya ardhi inayovitafuna vijiji hivyo na mingi watumiwa walikuwa ni wenyeviti wa vijiji na Halmashauri zao.

Hivyo, amewataka wote walioapishwa kwenda kuwa chachu ya suluhisho la migogoro hiyo na kuhakikisha wananchi wanakuwa wamoja katika kushiriki shughuli za maendeleo.

“Tuna migogoro na malalamiko mengi ya wananchi huko vijijini, tambueni ninyi kama viongozi, mna wajibu wa kuitisha vikao na mikutano na wananchi ili kuitafutia ufumbuzi migogoro hiyo. Mingi mna uwezo wa kuitatua, lakini pia hakikisheni mnahamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yenu,” amesema Msigala.

Advertisement

“Ni wajibu wenu pia kukemea vitendo vya rushwa na ninyi pia msijihusishe na vitendo hivyo, hakikisheni mnamsaidia Rais wetu, kusimamia maendeleo, tunataka kuwaonyesha wananchi wa Moshi kuwa hawakukosea kuwachagua ninyi,” alisema.

Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri hiyo, Juma Tukosa amewataka Viongozi hao kuandaa vipaumbele vyao watakavyokwenda kuvitekeleza ndani ya miaka mitano watakayokuwa madarakani.

“Tambueni kuwa pamoja na kiapo hiki, mtasaini mikataba itakayoonyesha katika kipindi cha miaka mitano mtafanya nini, hivyo hakikisheni Disemba mnaandaa vipaumbele vyenu kwa kuwa Januari 2020, mtajaza mikataba ya utendaji kazi na tutaifuatilia ili kuona mlichoandika katika mikataba kama kimetekelezeka,” amesema Tukosa.

Halmashauri hiyo ina jumla ya vijiji 157 na vitongoji 700 na vyote vimechukuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Advertisement