Wanafunzi 10 Umbwe Sekondari wasimamishwa masomo, Jafo akemea ubaguzi

Moshi. Wakati wanafunzi kumi wa Shule ya Sekondari ya Umbwe wakisimamishwa masomo kutokana na vurugu zilizotokea katika shule hiyo, Waziri Seleman Jafo amekemea ubaguzi na mateso kwa wanafunzi, akibainisha kuwa Serikali haitavumilia walimu wakuu wanaotajwa kuwa na tabia hizo.

Jafo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa Umbwe mkoani Kilimanjaro baada ya kuibuka vurugu usiku wa kuamkia Agosti 10 na kusababisha baadhi ya wanafunzi kujeruhiwa.

Kutokana na hali hiyo, Jafo alimtaka mkuu wa mkoa, Anna Mghwira kufanya uchunguzi shuleni hapo ili kubaini ukweli.

Katika vurugu hizo, wanafunzi sita walijeruhiwa na miundombinu ya shule kuharibiwa.

Katika maelezo yake, Jafo alisema amepata taarifa kuwa katika shule hiyo wanafunzi wa kidato cha sita wanawafanyia manyanyaso wa kidato cha tano, jambo alilosema kuwa hawezi kulifumbia macho na kuulaumu uongozi wa shule kwa kushindwa kulidhibiti.

“Sitaki kusikia unyanyasaji wowote wa wanafunzi ndani ya shule za sekondari, au ubaguzi wa dini, kabila wala rangi. Ikibainika katika shule yoyote kuna vitendo vyovyote vya ajabu, hatutamuhamisha mkuu wa shule. Tutamuondoa katika nafasi hiyo, kwa kuwa ameshindwa kusimamia shule,” alisema.

“Endapo tutasikia matatizo katika shule yoyote na uongozi umeshindwa kusimamia na nidhamu imekosekana; watu wananyanyasana, tutachukua hatua za haraka maana unyanyasaji huo unaweza kuleta athari kubwa na kupandikiza mbegu mbaya.

“Ninaomba niseme wazi, sitaki kumung’unya maneno. Hapa uongozi wa shule, umezembea kwa kiwango kikubwa. Madhara yanayotokea sasa hivi mkuu wa shule na timu yako kama mngekuwa mmejipanga vizuri isingetokea wanafunzi kufanya maamuzi yao wenyewe.”

Waziri huyo ameanzisha timu 10 katika shule hiyo na kuzipa majina, kwa lengo la kujenga undugu kwa wanafunzi na kuondoa hali ya kubaguana kidarasa na kidini. “Nyinyi vijana wadogo mnaanza kubaguana? Hamfahamu maisha yenu hapa bado yana safari ndefu. Mtaenda katika mazingira ya kazi na mkitengeneza sumu ya uadui hapa ninyi na vizazi vyenu itaenda kuwagharimu, kwa kuwa tabia mliyoonyesha ni chafu sana,” alisema Jafo.

Kwa upande wake Mghwira aliwataka wanafunzi kuacha tabia hiyo ya kujengeana uhasama.

“Ni lazima tuing’oe hii mbegu ya chuki ambayo imejipandikiza shuleni hapa,” alisema.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Abdulshaku Mlokozi na Inocent Nkya, waliishukuru Serikali kwa msamaha walioutoa na kuahidi kubadilika na kuondokana na hali ya ubaguzi na chuki.

Kozi kusitishwa KCMUCo

Wakati huo huo, mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Gilead Masenga amesema usitishwaji wa udahili wa baadhi ya kozi katika chuo cha tiba cha KCMUCo uliofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU) kwa miaka miwili iliyopita, umepoteza madaktari bingwa 200.

Dk Masenga alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa hosteli mpya za wanafunzi, maabara na uzinduzi wa makazi ya nyumba za kuishi za wachungaji uliofanywa na mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fedrick Shoo.

“Hapo mwanzo TCU ilisimamisha kozi karibu zote za uzamivu, lakini sasa wamefungua kozi mbili za upasuaji na mifupa. Hizi idara nyingine bado kutokana na maelekezo tuliyopewa na Tume ya uhaba wa wataalam,” alisema.

“Usitishwaji wa kozi katika chuo chetu ulikuwa na athari kubwa kwa sababu hapa KCMC kila mwaka tunazalisha madaktari bingwa 100 katika fani mbalimbali. Kwa hiyo kuzuiwa kwa miaka miwili tumepoteza madaktari bingwa 200 nchini,” alisema Dk Masenga.