HESLB Majina waliopata mikopo 2019/2020 haya hapa

Muktasari:

Hatimaye hofu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza walioomba mkopo kwa mwaka 2019 hadi 2020 kukosa mkopo itapungua baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutangaza orodha ya awamu ya kwanza waliopata mkopo.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania imesema wanafunzi 30,675 kati ya wanafunzi 45, 000 wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/20 walioomba mkopo kwa awamu ya kwanza wamepata.

Alizungumza leo Alhamisi Oktoba  17, 2019, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru amesema jumla ya Sh113 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao na fedha ambazo Serikali imeshaikabidhi bodi hiyo  ni Sh125 bilioni.

Amesema kati ya orodha hiyo wanafunzi wa kike ni 11,043 sawa na asilimia 36 na wakiume ni 19,632 sawa na silimia 64.

Hata hivyo,  amesema orodha ya awamu ya pili itatangazwa Oktoba 25,2019 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi ya mikopo kutoka kwa wanafunzi waliochelewa kukamilisha taratibu za udahili na kurekebisha maombi yao ya mkopo mtandaoni.

Amesema fedha za wanafunzi ambao wamefanikiwa kupata mkopo  zitatumwa vyuoni mapema kabla havijafunguliwa.

“Katika mwaka huu wa masomo Serikali imetenga kiasi cha Sh450 bilioni zinazolenga kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 128,285 ambapo kati yao zaidi ya wanafunzi 45,000 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo,” amesema.

Kuhusu makundi yenye uhitaji Badru amesema katika orodha ya kwanza wenye yenye wanafunzi 30,672, 6,142 ni yatima, wenye ulemavu ni 280 na wengine 277 wanatoka kaya zinazofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

“Katika makundi maalumu tuna wanafunzi 1889 sawa na asilimia sita ya wanafunzi 30,675 ambao walisoma shule binafsi lakini kutokana na hali duni ya uchumi walifadhiliwa na walithibitisha kwa kuweka nyaraka sahihi,” alisema.