Wanafunzi 585 wakatisha masomo kwa kupata ujauzito Ruvuma

Muktasari:

 

  • Idadi hiyo ya wananfunzi ni katika kipindi cha mwaka mmoja, mkuu wa mkoa asema hatua zimeanza kuchukuliwa kukabiliana na suala hilo huku kesi kadhaa zikiwa mahakamani

Songea. Wanafunzi 585 mkoani Ruvuma wamekatisha masomo kutokana na kufukuzwa shule baada ya kubainika kuwa na ujauzito katika kipindi ncha mwaka 20017/2018.

Akizungumza jana na Mwananchi, ofisa elimu mkoa, Ephaim Simbeye alisema idadi ya wanafunzi waliopata mimba mwaka 2017 ni 284 na mwaka 2018 walikuwa 301.

Alisema kesi 128 zimefikishwa mahakamani na kati ya hizo, 38 ni za mwaka 2017 wakati mwaka 2018 kesi 90 zimepelekwa mahakamani.

Alisema wataanza kutumia mahakama inayohamishika kusikiliza kesi hizo.

Simbeye alisema mikakati ya kuondoa au kupunguza tatizo hilo ni kwa shule za msingi na sekondari kuwa kuwapima mimba wanafunzi pindi wanapotoka likizo na kila baada ya miezi mitatu.

Alisema hatua hiyo itanusuru mikondo zaidi ya minne ambayo inapotea kila mwaka kwa tatizo la mimba.

Ofisa elimu huyo alisema mkakati mwingine unaotumika ni kuwatumia watumishi wa idara ya afya kupita shuleni na kutoa elimu ya afya kwa wanafunzi ili wajitambue na kutimiza ndoto zao.

Mganga mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Wendy Robert alisema bado kuna tatizo kubwa la mimba za utotoni wilayani humo na watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 ambao wamejifungulia hospitalini hapo mwaka 2015/2016 ni 137, mwaka 2016/2017 watoto 576 na 2017/2018 watoto 823.

Ofisa maendeleo ya jamii wa shirika linalojihusisha na masuala ya watoto, Victor John alisema ili kupunguza au kuondoa mimba za utotoni ipo haja ya kuangalia sababu za watoto kufikia hatua hiyo.Alisema hatua hiyo itawarahisishia kujua nini kifanyike.

Baadhi ya mambo yanayochangia hali hiyo ni umbali wa makazi wanayoishi na shule, hali duni kiuchumi, mila na desturi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme alisema wameanza kuchukua hatua kwa vitendo hivyo na kampeni aliyoanzisha Januari mwaka jana ya “Magauni Manne Niacheni Nisome”, imeongeza ufahamu wa vijana kujua madhara ya mimba za utotoni, faida ya elimu pamoja na hasara za kupata mimba.

Akifafanua alisema gauni la kwanza ni sare ya shule, la pili ni joho la mahafali, la tatu ni vazi la harusi na la nne ni la ujauzito.

Mmoja wa wanafunzi waliohitimu katika Sekondari ya Frank Weston wilayani Tunduru ambaye ana mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi minne, alishindwa kuzuia machozi aliposimulia mkasa uliompata.

Alisema vishawishi, marafiki na kutojitambua ndivyo vilivyomharibia maisha na kukatisha masomo yake.

“Naomba kama kuna shirika au taasisi zinisaidie nirudi shule kuendelea na masomo yangu. Nimejifunza na ninaahidi sitajihusisha tena na mapenzi,” alisema.

“Ni vishawishi tu ndivyo vimesababisha kukatisha masomo yangu ninajuta, maisha ni magumu.”

Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Mgomba, Zainab Kais alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, wazazi wajitahidi kuwaelimisha watoto wao madhara ya kujamiiana wakiwa na umri mdogo na pia kuwalipia madeni kwenye nyumba za kupanga, lakini jambo la muhimu, waache kuwatelekeza.

Zainab alisema mila na desturi potofu pia zinachangia watoto wa kike kupata ujauzito kwani wanafundishwa kuwa na wanaume wengi na namna ya kuwahudumia, hali ambayo inachangia wapoteze muda mwingi kujadili au kufanya mapenzi kuliko masomo.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani alisema malezi, makuzi pamoja na mila na desturi zimekuwa changamoto kwa watoto ambao wanajiingiza mapema kwenye mahusiano.

Wahukumiwa

Katika hatua nyingine, mahakama ya wilaya imewahukumu watu wanne kwenda jela miaka 30 na wengine kuchapwa viboko baada ya kukutwa na makosa ya kuwapa mimba wanafunzi.

Hakimu Odira Amworo alisema takwimu zinaonyesha kuwa kesi 11 za mimba za utotoni zilifunguliwa mwaka 2017 na zote zilisikilizwa na watu wanne walihukumiwa kifungo.

Kati yao Hamis Zawadi na Safari Mkwanda walihukumiwa miaka 30 jela, huku Juma Ally Pesama (25) mkazi wa Nalasi, Tunduru akihukumiwa adhabu ya viboko sita.

Mwingine, Cloud Mbanga (28), mkazi wa Mhuwesi alihukumiwa adhabu ya viboko 12 na watuhumiwa wawili walishinda kesi zao.