Wanafunzi UDSM wamwomba Rais Magufuli kuingilia vurugu za Afrika Kusini

Muktasari:

  • Viongozi wa Afrika wameombwa kukutana na watumie busara kujadili suluhisho la mgogoro wa ubaguzi ambao umekuwa ukijitokeza nchini Afrika Kusini.

Dar es Salaam. Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) nchini Tanzania kimelaani vikali mashambulio ya kibaguzi yaliyotokea nchini Afrika Kusini kwa watu wa mataifa mengine ya Afrika  huku wakimtaka Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kuingilia kati mzozo huo.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Septemba 12,2019 na Waziri wa Habari, Mawasiliano wa Daruso, Judith Mariki iliwaomba viongozi wa Afrika kukutana na kutumia maarifa na busara ili kudhibiti vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha maadili, mila na ubinadamu.

“Tunatoa wito kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Sadc, kuitisha mkutano wa dharura ili ujadili na viongozi wenzake kujadili mwafaka wa hali hiyo, ili kuwaleta pamoja kwa amani, kabla hali haijawa mbaya zaidi isipodhibitika,” alisema Mariki.

Alisema matukio hayo ya kinyama yanaharibu umoja na mshikamano wa Kiafrika kwa kuwa Waafrika wamekuwa wakiishi kama ndugu na kwa amani tangu wakati wa mapambano ya uhuru.

“Tusiruhusu mgawanyiko kutokana na tofauti zetu kwa sababu tunatokea nyumba moja kwa nini tugombee kipande cha mkate? Tunatoka bara moja kwa nini tuwadhalilishe ndugu zetu? Waafrika ni ndugu, ni walinzi wa ndugu zetu, mwafrika hawezi kuwa mgeni kwenye ardhi ya Afrika. Acha ubaguzi Afrika,” alisema Mariki.

Aliongeza, “Afrika ni kwa ajili ya Waafrika, tuache kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu tokea Afrika, umoja hautashindwa. Mungu ibariki Afrika, Mungu wabariki Waafrika.”