Wanafunzi wamfichua mwalimu aliyekuwa akiishi kinyumba na mwenzao

Buchosa. Mwalimu mmoja wa shule ya Sekondari Iligamba Halmashauri ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza (jina linahifadhiwa) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumtorosha na kuishi kinyumba na mmoja wa wanafunzi wake.

Hili ni tukio la pili kwa mwalimu kukamatwa akiishi kinyumba na mwanafunzi baada ya lile la mwalimu kumuoa na kuishi na mwanafunzi miaka miwili kuanzia mwaka 2016 hadi Agosti 20, 2018, gazeti hili lilipofichua suala hilo na kufanikisha mwanafunzi huyo aliyefaulu mitihani ya kidato cha nne kurejeshwa shuleni.

Akizungumzia kukamatwa kwa mwalimu huyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema kukamatwa kwa mwalimu kulitokana na taarifa kutoka kwa raia wema wakiwemo baadhi ya wanafunzi baada ya mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha nne kutoonekana shuleni kwa muda wa wiki moja.

“Mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo kidogo cha polisi Nyehuge kwa mahojiano zaidi,” alisema Kipole

Akionyesha kuchukizwa, mkuu huyo wa wilaya alisema, “sijui walimu wameingiliwa na jambo gani; wapo wanawake wengi wanaoweza kuwa nao kwenye mahusiano lakini wanawavamia wanafunzi. Hili halivumiliki na lazima tuchukue hatua kali za kinidhamu na kisheria,” alisema.

Siri ilivyofichuka

Kwa muda wa wiki moja, mwanafunzi huyo wa kidato cha nne anayedaiwa kuishi kinyumba na mwalimu wake hakuonekana shuleni ndipo wanafunzi wenzake walipoamua kufuatilia kujua mahali alipo.

“Baada ya kuchunguza tuligundua kumbe anaishi nyumbani kwa mwalimu ndipo tukafichua siri hiyo na kufanikisha mtego wa kumkamata mwalimu,” alisema mmoja wa watoa taarifa kwa sharti la kutotajwa jina

Mmoja wa wanafunzi wa kike shuleni hapo aliliambia Mwananchi kuwa mwalimu huyo ana tabia ya kuwataka na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike, tabia inayodaiwa kuwakera baadhi ya wanafunzi ambao baada ya kugundua alikuwa akiishi kinyumba na mwenzao waliamua kutoa siri.

“Arobaini zake zimefika; tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike siyo tu dhidi ya mwalimu huyu pekee, bali kwa walimu wote kubaini wenye tabia ya kuwataka na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi ili hatua za kisheria zichukuliwe kukomesha tabia hii,” alisema mwanafunzi mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa

Mkuu wa shule, ofisa elimu

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mkuu wa shule ya Sekondari Iligamba, Siraji Kalyango alisema mwalimu huyo alikamatwa Januari 17, 2020 akiwa chumbani kwake na mwanafunzi huyo.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Buchosa, Bruno Sangwa, alisema kwamba vitendo vya walimu kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao si tu havivumiliki, bali pia vinatia doa haiba na heshima ya kazi adhimu ya ualimu na sekta mzima ya elimu.

“Vitendo hivi havivumiliki. Tunaviachia vyombo vinavyohusika vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema Sangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda alisema ofisi yake haitafumbia macho vitendo vyovyote vinavyokwamisha juhudi za Serikali za kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.

Tukio linalofanana na hilo

Agosti 20, 2018, gazeti la Mwananchi lilifichua habari za mwalimu mmoja wilayani Sengerema kumuoa mwanafunzi wake muda mfupi tu baada ya kumaliza mitihani ya kuhitimu kidato cha nne.

Hata baada ya matokeo kutoka na mwanafunzi huyo kuwa miongoni mwa wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na sita, bado mwalimu huyo aliendelea kuishi naye kama mume na mke huku akimhamishia jijini Mwanza kama sehemu ya kuficha suala hilo.

Baada ya habari hiyo ya uchunguzi kuripotiwa na gazeti hili, Serikali iliingilia kati na kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo ambaye matokeo yake ya majaribio muhula uliopita yalionyesha kuwa maendeleo yake ni mazuri kwa kupata ufaulu wa daraja la pili.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyehunge anakosoma mwanafunzi huyo, Boniphace Kafumu alisema kwamba kwa matokeo hayo, mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) alishika nafasi ya 20 kati ya wanafunzi 50 wa darasa la mchepuo wa HKL (Historia, Jiografia na Lugha).