Wanamuziki bendi ya Sky Melodies wapata ajali mkoani Singida

Thursday August 22 2019

Sky Melodies,Hospitali ya Mkoa wa Singida,mwananchi, habari mwananchi, Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Sweetbert Njewike

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wanamuziki wa bendi ya muziki wa dansi ya Sky Melodies inayoongozwa na Nico Millimo wamepata ajali leo Alhamisi  Agosti 22, 2019 katika kijiji cha Sepuka Mkoa wa Singida wakiwa wanatoka katika mkesha wa Mwenge.

Akizungumza na Mwananchi leo, Millimo amesema chanzo cha ajali ni gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Hiace kupata hitilafu katika tairi na kupoteza mwelekeo.

“Tumepata ajali tukiwa tunatoka kijiji cha Sepuka mjini Singida. Tulikuwa  tunatoka katika mkesha wa Mwenge na bendi yetu ilikuwa huko kutoa burudani,” amesema.

Ameongeza, “Tunawaondoa watu wasiwasi na ajali yetu haihusiani na ulevi kama picha zinavyoonekana kuwa kuna makreti ya bia na chupa zake, zile ni za binti wa mratibu wa shughuli za tulikokuwa, alikwenda kuuza vinywaji hivyo sisi tulimpa lifti ili tumshushe Singida mjini.”

Amebainisha kuwa katika gari hilo walikuwa 10 na wote walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Singida, akibainisha kuwa kati yao watatu wameumia zaidi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Sweetbert Njewike amesema hana taarifa za ajali hiyo.

Advertisement

 

 

 


Advertisement