Wananchi Mwanza wanavyosotea vitambulisho vya Taifa

Wananchi wakiwa kwenye foleni katika ofisi za Nida wilaya ya Nyamagana kwa ajili ya kupata namba. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

Desemba 27, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli alitangaza kuongeza siku 20 zaidi kuanzia Januari 1 hadi 20, 2020 kwa ajili ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole huku akitoa maagizo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya siku hizo kuisha laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa zizimwe.

Mwanza. Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamemuomba Rais wa Tanzania, John Magufuli kuingilia kati na kuongeza muda wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Wananchi hao wametoa kilio hicho leo Ijumaa Januari 17, 2020 ikiwa zimebaki siku nne kabla ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzizima laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa.

Msingi wa ombi hilo unatokana na kile walichodai kwa muda huo uliobaki hawawezi kupata namba au vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo, awali TCRA ilitangaza kuzifungia laini ambazo zisingekuwa zimesajiliwa hadi Desemba 31 mwaka 2019 lakini Rais Magufuli aliongeza siku 20 zaidi kuanzia Januari 1 hadi 20, 2020 na kuagiza TCRA baada ya siku hizo kumalizika zizimwe.

Leo Ijumaa katika ofisi za Nida Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Mwananchi limefika katika kuangalia shughuli ya uandikishaji vitambulisho vya Nida na kushuhudia umati mkubwa wa wananchi waliojipanga foleni.

“Iwapo laini za simu zitafungwa watu wengi watapata shida sana, tunategemea maisha yetu kupitia simu, mtu ana kibarua anategemea kwenda kupandisha tofali anajulishwa kupitia simu saa kama hana mawasiliano hali itakuwa mbaya, huenda ajira nyingi zikapotea,” alisema Gerald Kayoko mkazi wa Buhongwa

Naye Astelia Anas amesema, “ukiangalia wananchi tunanyeshewa hata mvua hakuna sehemu ya kujikinga na foleni ni kubwa sana, hata fomu zinalowana unaanza kujiandikisha upya  kwa kweli hali ni mbaya sana tunaomba tusaidiwe.”

Mwingine Tatu Olimpia amesema badala ya wananchi wote kukaa hapo kunyeshewa mvua na jua ni bora Nida ikatoa taarifa kwamba kwa siku itaweza kuhudumia watu kadhaa kwa siku ili wengine ambao hawataweza kuhudumiwa kwa siku husika waondoke kuliko kupoteza muda.

“Unafika saa kumi usiku unakaa mara jua mara mvua,  inafika jioni hata hupati huduma kwa hiyo unapoteza muda na namba hauipati, hakika tunateseka sana,” amesema

Diwani viti maalum Manispaa ya Ilemela, Denisa Pagula naye aliungana na wananchi hao akisema ingetumika busara zaidi kuongeza muda ili watu wasiathirike katika huduma.

Naye Mkuu wa Mkao wa Mwanza, John Mongella aliyetembelea ofisi za Nida Mkolani kujionea hali ilivyo, aliwataka wananchi hao kuwa watulivu kwamba hakuna mtu atakayebaki bila kusajiliwa “kikubwa ni kuvumiliana kulingana na changamoto zinazojitokeza.”