Wananchi Tarime wadaiwa kuwashambulia polisi, watumishi kwa mawe, mishale

Muktasari:

  • Watumishi wawili wa idara ya ardhi na askari polisi washambuliwa na wananchi wakati wakipima mpaka wa kijiji cha Murito na Gibaso wilayani Tarime Mkoa wa Mara nchini Tanzania.

Tarime. Askari wa Jeshi la Polisi na watumishi wawili idara ya ardhi halmashauri ya wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara nchini Tanzania wamelazwa hospitali ya wilaya ya Tarime mkoani humo baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wananchi.

Watatu hao wameshambuliwa jana Ijumaa Aprili 3,2020 wakati wakipima mipaka ya utawala ya vijiji vya Murito na Gibaso.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Aprili 4, 2020, Mganga mkuu wa wilaya ya Tarime, Kelvin Mwasha amesema majeruhi hao waliwapokea jana jioni wakiwa katika hali mbaya kutokana na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Amesema ofisa mpima ardhi Joseph Mulazi amekatwa kichwani, kifua kwa kutumia vitu vya ncha kali, mwingine ni Sylivatus Mafuru naye kaumizwa maeneo mbalimbali na askari polisi kakatwa mgongoni na mkono wa kulia.

Amesema wanaendelea na matibabu kutokana na majeraha hayo na kuwa watatibiwa hapohapo.

Ofisa mtendaji wa kata ya Kwihancha, Daud Matiko amesema yeye alipigwa jiwe kwenye nyonga na kupata matibabu zahanati na kuruhusiwa kuondoka.

"Wakati tunazunguka kupitia maeneo mbalimbali ghafla wananchi walitupigia yowe na kuanza kutushambulia kwa mawe, mishale na mapanga, askari wawili waliokuwa na silaha walitumia hekima kubwa kutofyatua risasi vinginevyo wangetuua maana walikuwa wametuzingira," amesema.

Amesema wakati wanawashambuliwa walikuwa wanadai ni bora kuwaua maana wanajidai ndiyo wanatumwa na serikali kubadili mipaka yao.

Kamanda wa mkoa wa kipolisi Tarime Rorya, William Mkondya amesema hakuwa na taarifa kwa kuwa yuko Mwanza huku akiahidi kufuatilia suala hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri amesema alifika eneo la tukio na kuahidi wahusika wasakwe, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mjibu wa mmoja wa wananchi wa Murito amesema mgogoro wa mpaka wa kijiji hicho na Gibaso ni wa muda mrefu na chanzo ni misingi ya koo za Wanyamongo na Wairegi.