Wananchi waeleza Tasaf ilivyowainua kiuchumi

Muktasari:

Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) wameelezea namna walivyonufaika na mfuko huo katika kujiinua kiuchumi.

Dar es Salaam. Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) wameelezea namna walivyonufaika na mfuko huo katika kujiinua kiuchumi.

Wakizungumza leo Jumatatu Februari 17, 2020 katika uzinduzi  wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf, wanufaika hao wamesema yapo mabadiliko mengi kiuchumi kwa kaya masikini zilizosaidiwa.

Mwakilishi wa wanufaika hao, Asha Mohamed Ally kutoka Bagamoyo mkoani Pwani amesema kaya zao zimemudu mahitaji  muhimu ya watoto shuleni, kujenga nyumba,  vyoo bora na kuweka mahitaji ya msingi  kama maji na umeme.

“Kaya zetu zimehamasika kuwapeleka kliniki watoto chini ya miaka mitano na kuzingatia lishe bora,” amesema Asha.

Mnufaika huyo amesema wanapata matibabu  kupitia bima ikiwamo Bima ya Afya ya Jamii (CHF).

Amesema kaya nyingi zimeweza kuanzisha shughuli za kiuchumi kama kilimo, ufugaji na biashara baada ya kupewa mafunzo ya ujasiriamali kupitia mfuko huo.

“Tumehamasishwa kujiunga kwenye vikundi vya uchumi na tumejifunza namna ya kutengeneza miradi mbali mbali,” amesema Asha.

Mnufaika huyo amesema wameshiriki kwenye ajira za muda zikiwamo za kuboresha miundo mbinu ya barabara na utunzaji wa mazingira.

“Ombi letu kwako ni kwamba mpango huu uendelee kwa wenzetu wenye hali duni kiuchumi na ambao hawakufikiwa kwenye hatua ya kwanza,” amesema Asha.