UCHAMBUZI: Wananchi wamepata chama mbadala cha siasa nchini?

Watanzania bado wapo katika giza nene, wanapofanya jitihada za kupata chama cha siasa mbadala, licha ya kuwa na fursa hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Itakumbukwa uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais wa kwanza kuhusisha vyama vingi baada ya mfumo huo kuruhusiwa mwaka 1992, ulifanyika mwaka 1995.

Pamoja na chama tawala CCM, vyama vingine vilivyoshiriki ni chama cha Wananchi CUF, NCCR-Mageuzi na UDP. Kwa awamu ya sita tangu uchaguzi huo ufanyike, mwaka huu Tanzania inatarajiwa kuchagua viongozi hao wa kisiasa katika ngazi ya Taifa, Oktoba.

Tofauti na mwanzo, vyama mbadala vilikuwa vitatu, awamu hii inatarajiwa vyama 19 vitashiriki huku 18 kati ya hivyo vikitazamiwa kuwa mbadala wa CCM.

Sayansi ya Uchaguzi inaelekeza, katika mfumo wa vyama vingi ni muhimu kabla ya muda wa uchaguzi mkuu haujawadia, kuwe na vyama angalau viwili vyenye sifa za kuvipa hadhi ya kuwa mbadala wa chama tawala.

Pamoja na mambo mengine, ili chama kipate hadhi hiyo, kinatakiwa kiwe kinafahamika vizuri, kinaeleweka na kuaminiwa na wananchi ambao ndiyo wapiga kura. Hakuna muujiza wa kuwezesha chama kuaminika, bali ni chenyewe kihakikishe wananchi wanakielewa, wanakiamini kutokana na namna kinavyotekeleza majukumu yake ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kisera kwa ubora zaidi ya chama tawala.

Hutarajiwa vyama hivyo mbadala vijiweke katika hali ya kuaminiwa na wananchi, kabla ya uchaguzi mkuu ili wapiga kura wavitofautishe na kuviweka kwenye mizani, kabla hawajaamua chama kipi kipewe dhamana ya kuongoza Serikali.

Ikumbukwe, mfumo wa uchaguzi nchini hautoi nafasi kwa mgombea binafsi; ili mtu agombee udiwani, ubunge au urais lazima awe chini ya mwavuli wa chama cha siasa.

Bila shaka hilo linadhihirisha umuhimu wa kwa nini chama cha siasa kinatakiwa kufahamika na kuaminiwa na wananchi, kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Hoja hapa ni je, Watanzania wanapotizama vyama 18 ambavyo ni mbadala wa chama tawala, wanaona mwanga?

Kwa namna vyama vinavyojiendesha kwa maana ya kuandaa sera, ilani na miongozo mbalimbali katika kujiimarisha na kuwajengea wananchi matumaini.

Mfano halisi unabainika katika nyaraka muhimu za vyama hivyo. Ili kudhihirisha hilo, leo zinarejewa baadhi ya sera za CCM na zile za chama kikuu cha upinzani Chadema, ili kupima na kutathmini sera hoja.

Mathalani, Sura ya Tatu ya Ilani ya uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 na Sura ya pili ya Sera za CCM za Mwaka 2010 – 2020, zinaeleza kuhusu maendeleo katika miundombinu ya barabara, bandari, reli na anga. Sera hizo zinaeleza kuwa utafanyika ujenzi mkubwa wa reli ya kisasa ili kuendana na mahitaji ya wakati, ambayo itatoka Dar es salaam mpaka Mikoa ya Mwanza na Kigoma.

Pia inaeleza kuwa reli ya kati, Tazara, Tanga na Moshi zitafanyiwa ukarabati huku ile ya mikoa ya kusini, yaani Lindi na Mtwara ikielezwa kuwa itajengwa.

Sababu na malengo ya utekelezwaji wa hatua hizo pia unaelezwa kuwa ni kuchochea kukuwa kwa uchumi, kupitia usafiri na usafirishaji wa mizigo.

Katika sekta ya afya, CCM kimeweka nia ya kujenga vituo vya afya kila kata na zahanati kwenye kila kijiji, kwa kutumia makusanyo ya ndani na ili kurahisisha huduma, kimeandaa utaratibu wa bima za afya kwa jamii (CHF) kwa bei nafuu ambapo Mfumo huo unaruhusu familia yenye watu sita, kulipa Sh30, 000 kwa ajili ya wote kuhudumiwa katika baadhi ya hospitali huku kukiwa na utaratibu unaowezesha wazee wote nchini, kutibiwa bure, licha ya hivyo kuna ujenzi wa hospitali za rufaa kila kanda na ununuzi wa vifaa vya kisasa.

Kwa upande wa Sera za chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema, ambazo zilizinduliwa Mwaka 2018, zinazungumzia pia masuala ya sekta ya miundombinu na nishati.

Kuhusu miundombinu ya barabara, reli, na maji, sera hizo zinaeleza kwa ufupi kuwa, itaboreshwa.

Kwa mfano inaeleza kuwa reli itaboreshwa iwe ya kisasa, bila kubainisha aina ya usasa unaoelezwa na wala kuonyesha tofauti kati ya hali ilivyo na itakavyokuwa baada ya utekelezwaji wa sera hiyo.

Sura ya Saba ya sera hizo, inaeleza kuwa yatafanyika maboresho kwenye sekta ya afya, kwa kutumia sekta binafsi na kwamba serikali itakuwa muangalizi yaani Chama kitatumia sera za Kibepari katika masuala ya afya, bila shaka hii ni kutokana na itikadi ya Chadema kuwa ni ya kipebari yenye mrengo wa Kati (Center Party), biashara na soko huru kwa sekta zote ikiwemo ya afya.

Katika mazingira ya hivyo, ambapo chama tawala kinafanya bidii zinazodhihirika wazi kuwa kinalenga kukidhi matakwa ya wananchi, ni dhahiri kuwa vyama mbadala, vinahitaji kuwa na watafiti wabobevu wa kuangalia mahitaji na matamanio ya wananchi ambayo hayajafikiwa na sera za chama tawala.

Vinginevyo, sera za vyama hivyo zitaendelea kuwa dhaifu, zisizo na manufaa yanayotosha kuvipa hadhi ya kuwa vyama mbadala wa chama tawala.

Ili kuleta ushindani wa kisiasa wenye tija, sera mbadala zinapoundwa, zinatakiwa kueleza majibu yanayokosekana kwenye sera za chama tawala. Katika sayansi ya utafiti wa sera za vyama vya siasa hasa kwa upande wa vyama mbadala, zinatakiwa kuwa sera dadavuzi, zenye kujipambanua na kujitofautisha kwa kuwa na mwonekano chanya kwa wananchi dhidi ya zile za chama tawala. Suala hilo linatakiwa kuzingatiwa zaidi kwenye mazingira ambayo chama tawala kinakuwa na mifumo imara katika nyanja karibia zote, kikitiwa chachu kwa kuwa na viongozi wanaoyaishi maneno yao.

Kinyume chake, vyama vinavyotakiwa kuwa mbadala huelekea kukosa sera zenye nguvu za kuviwezesha kusimama mbele ya wananchi, ambapo hatua hiyo ikifikiwa huitwa mwanguko wa vyama kisera, hali inayohitaji msaada wa haraka kuviwezesha kurudi kwenye ushindani kama hali ilivyo sasa katika vyama mbadala nchini.

Mwandishi ni mchambuzi wa Siasa na Maendeleo nchini anapatikana kwa simu 0742102913