VIDEO: Wananchi watofautiana sakata la Lugola kumuonya Musiba

Muktasari:

Baadhi ya wananchi wametofautiana  kitendo cha Waziri wa  Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumuonya mtu anayejiita ‘mwanaharakati huru’,  Cyprian Musiba akimtaka kuacha tabia ya kuwachafua viongozi na watu mbalimbali kwa madai kuwa ametumwa na Serikali.

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wametofautiana  kitendo cha Waziri wa  Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumuonya mtu anayejiita ‘mwanaharakati huru’,  Cyprian Musiba akimtaka kuacha tabia ya kuwachafua viongozi na watu mbalimbali kwa madai kuwa ametumwa na Serikali.

Wakati Lugola akieleza hayo, Musiba alimjibu akibainisha kuwa yupo tayari kukamatwa, kuwekwa mahabusu au kufungwa jela lakini hatoacha kumsemea Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Wananchi hao wametoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii ya Mwananchi ya Twitter na Facebook.

Deo Mfuse ameandika, “Kuna wakati nilitamani utoe neno kuhusu huyu jamaa lakini bahati mbaya hatukusikia  hilo neno toka kwako. Elewa kila jambo lina wakati.”

Ramson Issa alimpongeza Lugola kwa hatua hiyo akisema kuwa mhusika atatii onyo hilo na kwamba hakuna aliye juu ya sheria.

Mentali H Mentali ameandika, “Yote haya kwa vile jamaa anapekenyua ubunge jimboni mwa waziri mwaka 2020. Ukiona mfugaji wa nyuki ameanza kuwachukia nyuki ujue wameshamtoa manundu.”

Norbert Kagali amesema, “Wanapimana misuli kati ya waziri na mwanaharakati tunasubiri kuona nani zaidi ya mwenzake na hapo itajulikana nguvu inatoka wapi.”