Wanaocheza michezo ya kubahatisha kupita kiasi kupewa tiba

Muktasari:

Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania inaandaa utaratibu wa kuanza kutoa tiba kwa wanaopata uraibu kutokana na kucheza mchezo huo kupita kiasi.

Dodoma. Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania inaandaa utaratibu wa kuanza kutoa tiba kwa wanaopata uraibu kutokana na kucheza mchezo huo kupita kiasi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 13, 2019 na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la mbunge wa Ileje (CCM), Janeth Mbene.

Mbene amesema michezo hiyo inaingiza pato kwa Taifa lakini ina athari kubwa za kimaadili na kisaikolojia kama ilivyo dawa za kulevya, ikiwa haitaangaliwa kwa umakini.

“Serikali imechukua tahadhari zipi kuhakikisha michezo hii inashirikisha watu wenye ufahamu wa athari zake. Wapo wanaotegemea michezo hii jambo linaloweza kuwaletea athari kubwa za kiuchumi na kijamii,” amehoji naibu waziri huyo wa zamani wa Fedha na Mipango.

Katika majibu yake Dk Kijaji amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali zinazolenga kupunguza ushawishi wa kushiriki michezo ya kubahatisha kupita kiasi na kupunguza athari hasi zitokanazo na michezo ya kubahatisha kwa jamii.

“Hivi sasa kuna changamoto ya kusimamia wachezaji wa michezo ya kubahatisha, hususan wachezaji wa michezo isiyohusisha mfumo wa Tehama,” amesema.

Amesema Serikali ipo mbioni kuunganisha michezo yote kwenye mfumo wa Tehama unaoendelea kujengwa.

“Mfumo utaiwezesha Serikali kuratibu mienendo ya kila mchezaji na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria na kanuni za michezo ya kubahatisha,” amesema.

Amesema mfumo huo utatumika pia kudhibiti uchezaji uliokithiri kwa kuweka viwango vya fedha za kucheza. 

“Kwa michezo inayoendeshwa kwa mfumo wa kompyuta, usimamizi wa wachezaji unafanyika kwa kuwa taarifa za mchezaji huchukuliwa kikamilifu na hivyo Serikali inaweza kuwatambua na kuwasimamia kupitia taarifa zao,” amesema.

Amesema pale inapobainika kuwa mchezaji ameathirika kutokana na kucheza kupita kiasi hufungiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kwa kushirikiana na waendeshaji.

Amebainisha kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kuanza kutoa tiba kwa wachezaji waliopata uraibu kutokana na kujihusisha kupita kiasi katika mchezo huo.

Katika swali la nyongeza,  Mbene amesema kudhibiti mchezo huo si rahisi na kuhoji ni lini mafunzo yametolewa.

Akijibu swali hilo, Dk Kijaji amesema semina zinafanyika kwenye makundi mbalimbali  na katika kila eneo lenye michezo ya kubahatisha pamoja na  kusambaza majarida kuwaeleza athari ya kucheza kupita kiasi.

“Na kama burudani inachukua muda kidogo zaidi wajenge uchumi wao na Taifa kwa ujumla,” amesema.