Wanaodaiwa kumuua diwani, askari wa JWTZ wakamatwa

Tabora. Jumla ya watu ishirini na tatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora kwa makosa mbalimbali zikiwemo tuhuma za mauaji ya diwani na mwanajeshi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Laurian Fabian amesema leo Ijumaa Aprili 3, 2020 kuwa watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa diwani wa kata ya Usunga wilayani Sikonge, Alfred Masamalo aliyeuawa Machi 4, 2020.
Diwani huyo aliuawa baada ya kuvamiwa na watu akiwa nyumbani kwake usiku na kisha kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani.
Marehemu alikatwa pia mkono ulioanguka chini kutokana na kujikinga asikatwe kichwani na alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Pia jeshi hilo hadi sasa limekamata watuhumiwa sita ambao wanatuhumiwa kumuua askari wa kikosi cha 262 Milambo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati akielekea nyumbani kwake baada ya kutoka doria ya mtaani eneo analoishi Manispaa ya Tabora.
Mwanajeshi huyo aliuawa Machi 30, 2020 na mwili wake kukutwa umbali wa kilomita moja toka nyumbani kwake saa kumi na mbili alfajiri siku hiyo.
Wakati huo huo Jeshi hilo linawashikilia watu 13 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyang'anyi wa kutumia nguvu na silaha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora.
Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.