Wanaomba msamaha kuungama au wameamua kunyenyekea vyeo?

Rais John Magufuli ametangaza msamaha kwa wabunge watatu wa CCM ambao sauti zao za kwenye simu zilivuja wakimzungumzia vibaya. Ni January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama).

Rais Magufuli alitangaza msamaha kwa January na Ngeleja kwanza. Alisema walimwomba msamaha. Akasema ikiwa Mungu anasamehe, yeye nani asisamehe? Akaeleza kuwa angeweza kuwapeleka kwenye vikao vya maadili CCM ambako wangefukuzwa uanachama.

Ukipoteza uanachama, na ubunge ndio basi. Je, January na Ngeleja waliona dalili za kupoteza ubunge ndio maana waliamua kuomba msamaha? Au walitafakari na kuona makosa yao, ndio maana waliungama?

Nape akaonekana Ikulu alipokwenda kuomba msamaha. Je, naye alitafakari na kuona alimkosea sana Rais Magufuli kwa matamshi aliyotoa au alikwenda kwa vile January na Ngeleja waliomba na kusamehewa?

Je, Nape alijutia aliyoyasema dhidi ya Rais Magufuli au aliogopa baada ya kumsikia akizungumzia kupeleka suala la waliomtukana kwenye vikao vya chama?

Desemba 8, 1987, Rais wa 40 wa Marekani, Ronald Reagan aliposaini mkataba wa kuachana na silaha za nyuklia na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa iliyokuwa Dola ya Umoja wa Nchi za Soviet, Mikhail Gorbachev alitumia maneno ya Kiingereza – “trust but verify”. Kwa Kiswahili ni “amini lakini jiridhishe”.

Kwamba pamoja na kusaini mkataba, lakini Marekani ingeendelea kufuatilia ili kujiridhisha kama Soviet wangebaki na uaminifu kwenye mkataba. Si kuamini jumla.

Rais Magufuli alisema amemsamehe Nape akamtaka aende kutumikia wananchi na chama chake, alee na familia. Akasema “labda akengeuke tena”.

Tafsiri ya maneno hayo ya Rais Magufuli ni kuwa amepokea msamaha wa Nape lakini ataendelea kujiridhisha.

Na hapo ndipo tunapata aina za msamaha. Upo wa kusamehe na kusahau, yaani unasamehe jumla, hakuna kuangalia yaliyopita. Kwa vile mkosaji kakiri kosa na kaomba kusamehewa, basi unasamehe na kusahau. Kinachofuata ni kuganga yajayo.

Upo msamaha wenye angalizo. Unasamehe lakini unabakiza shaka ya kuendelea kuona kama mkosaji atarudia alichofanya. Anayesamehe hasemi yaliyopita si ndwele, bali anayaweka yaliyotokea jana kama akiba ya kuona kama mkosaji kweli amejirekebisha?

Ni msamaha wenye kutoa faida kwa aliyesamehewa, kuthibitisha kama kweli amemaanisha au geresha.

Kuna msamaha wa wito wa Mungu, kwamba Mungu anasamehe wakosaji, wewe binadamu ni nani hata usisamehe? Huu ndio msamaha ndani ya maneno ya mwandishi mashuhuri wa Uingereza, Alexander Pope Karne ya 18, aliyesema, “to err is human, to forgive divine.”

Kwamba kukosea ni asili ya binadamu, kusamehe ni sifa ya Mungu, hivyo mwenye kusamehe wenye kumkosea hutimiza sifa mojawapo ya Mungu.

Upo msamaha wa kuvunja ushirikiano au uhusiano. Unaitwa msamaha wenye kinyongo. Unasamehe anayekukosea lakini unaamua kutoendelea kufanya ushirikiano naye. Mathalan, Rais Magufuli angesema amewasamehe January, Ngeleja na Nape, lakini akataka wafutwe uanachama.

Ukipitia aina hizo za msamaha, Rais Magufuli amejitenga na msamaha wenye kinyongo. Ametaka waendelee kuwa wanachama wa CCM na ubunge wao. Ameonyesha moyo safi, ni jambo la kumpongeza.

Alipotangaza kuwasamehe January na Ngeleja, alibeba aina mbili za msamaha; kusamehe na kusahau, vilevile wito wa Mungu. Hakuweka angalizo la “wakirudia”, badala yake alimtaja Mungu kuwa husamehe. Alichagua kutimiza sifa ya Kimungu!

Zamu ya Nape ilipofika, upepo ukabadilika, akasema “labda akengeuke tena”. Kwa maana hiyo Rais amempa Nape faida ya kujiridhisha kuhusu ombi lake la msamaha kama atabaki mwaminifu au atarudia makosa.

Unaweza pia usikosee ukisema kuwa shaka hiyo ambayo Rais aliiweka wazi kwa Nape, ipo pia kwa January na Ngeleja. Kwamba hawajaaminika sana.

January na Ngeleja wanajutia makosa yao au wameomba msamaha kwa sababu sauti zilivuja? Nape pia ni kwa nini sauti yake kwenye simu ilisikika kabla ya January na Ngeleja, lakini wao waliomba msamaha kabla yake? Ameomba msamaha kwa dhati au kafuata mkumbo?

Swali kwa wote; wanamchukuliaje Rais Magufuli? Kama asingekuwa na mamlaka aliyonayo kwenye Jamhuri, serikalini na ndani ya chama, wangeona ulazima wa kumwangukia awasamehe?

Hapa pia Rais Magufuli ajiulize; wamemwomba msamaha kama John Magufuli, kaka yao/baba yao, au kwa sababu ni Rais na Mwenyekiti wa CCM? Na msamaha alioutoa, amejitazama katika nafasi ipi? Kama John Magufuli au Rais na Mwenyekiti CCM?

Ingetokea sauti zilizovuja, wangekuwa wanamzungumzia mkuu wa mkoa, wilaya au kiongozi yeyote chini ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge, jitihada za kuomba msamaha zingekuwa kubwa?

Maswali hayo ni ufunguo kuwa kumekuwa na hulka ya watu kuogopa na kuheshimu vyeo kuliko watu na utu wao. Ndiyo maana ipo sababu ya kujiuliza msamaha kama ni ungamo la moyoni au unyenyekevu wa vyeo?

Mwisho tujiulize, nani alivujisha sauti? Si tu kwamba alitenda uhalifu, lakini alimdhalilisha Rais Magufuli. Yale maneno yalibeba ujumbe gani? Kwamba jamii ijue namna ambavyo Rais ananangwa, ili iweje?

Kati ya mambo ambayo hayaepukiki duniani ni Rais kutetwa. Ni kiongozi wa umma. Watu watamteta kwa mitazamo yao, inaweza kuwa chanya au hasi. Hilo lifahamike. Dhambi ni kumvunjia heshima.

Dhambi kubwa zaidi ni kupekua simu za watu ili kutafuta Rais anavyotetwa. Ndani ya nyumba mama na watoto humteta baba. Majimboni wananchi humteta mbunge wao. Rais Magufuli anapaswa kuwachukia hata waliovujisha zile sauti.