Wanaotuhumiwa kumuua Dk Mvungi wamkataa hakimu

Muktasari:

Washtakiwa sita katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, Dk Sengondo Mvungi wamemkataa hakimu mwandamizi, Vicky Mwaikambo kwa madai kuwa hawana imani naye.

Dar es Salaam. Washtakiwa sita katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, Dk Sengondo Mvungi wamemkataa hakimu mwandamizi, Vicky Mwaikambo kwa madai kuwa hawana imani naye.

Wametaka shauri hilo kuhamishiwa kwa hakimu mfawidhi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo yamejiri leo Jumanne Januari 28, 2020 baada ya wakili wa Serikali, Ashura Msava kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, kwamba shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo mshtakiwa, Longishu Losindo alinyoosha mkono na kuieleza mahakama hiyo kuwa wapo mahabusu kwa muda mrefu, hakuna kinachoendelea katika shauri hilo.

"Shauri hili haliendi mbele tupo ndani kwa muda mrefu, hatuna imani na hakimu anayeendesha kesi yetu tunataka shauri hili lihamishiwe kwa hakimu mfawidhi wa mahakama hii," amedai Losindo.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo hakimu Mwaikambo amesema washtakiwa hao walitakiwa kuandika barua kwa mfawiidhi wa mahakama hiyo  kutokuwa na imani na hakimu huyo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Februari 10, 2020 kwa ajili ya kutajwa

Awali, kesi hiyo ilikuwa kwa hakimu mkazi mwandamizi,  Augustina Mmbando lakini washtakiwa hao  walimkataa na baadaye kuhamishiwa  kwa hakimu Augustine Rwezile ambaye  kwa sasa amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ndipo lilipopelekwa kwa hakimu Mwaikambo.

Mbali na Losindo washtakiwa wengine ni Msigwa Matonya, Mianda Mlewa, Paulo Mdonondo, Juma Kangungu na John Mayunga.

Katika kesi ya msingi washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji ikidaiwa kuwa Novemba 3, 2013 walifanya kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 .

Inadaiwa siku ya tukio katika eneo la Msakuzi Kiswegere  Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Mvungi.