Wanasheria wa kina Mbowe, Serikali wavutana kortini

Thursday October 17 2019

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kesho Ijumaa Oktoba 18, 2019  itatoa uamuzi iwapo mashahidi katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe watatoa ushahidi ama washtakiwa wenyewe.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa leo Alhamisi Oktoba 17, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomasi Simba baada ya kusikiliza hoja za upande wa utetezi ambao wanataka mashahidi ndiyo waanze kutoa ushahidi kabla ya washtakiwa huku upande washtakiwa ukiupinga utaratibu huo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kabla ya kuiwasilisha hoja zao, alidai kesi ilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza utetezi.

Akiwasilisha hoja, Nchimbi alidai ombi la upande wa utetezi  la kutaka kuanza kusikiliza ushahidi wa mashahidi kabla ya washtakiwa  halitekelezeki kwa sababu linakiuka sheria ya ushahidi, mwenendo wa mashauri ya jinai inayotoa mwongozo wa kuendesha na kusikiliza mashauri hayo.

Alidai kifungu cha 144 cha Sheria ya Ushahidi sura 6 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kinazungumzia uongozaji wa mashahidi.

Nchimbi aliendelea kudai wanashawishi mahakama kwamba utaratibu wa uwasilishaji mashahidi wakati wa utetezi unatamkwa na kifungu cha 231 (1) (a) na (b) pamoja na mambo mengine kinazungumzia haki na utaratibu wa kuwasilisha utetezi.

Advertisement

Hivyo mshtakiwa hawezi kuingia kwenye haki ya kuita mashahidi kama yeye mwenyewe hajaamua au hajatoa ushahidi.

Nchimbi aliiomba mahakama ijielekeze pia katika kifungu cha 38 (2) (a) na (b) kwani utaratibu wa utoaji wa ushahidi wa utetezi mahakama inapaswa kumuita mshtakiwa kama shahidi wakati akitoa utetezi wake.

Alibainisha washtakiwa wanavaa kofia mbili kwa wakati mmoja kwa kuwa kwanza wanasimama kama washtakiwa na pia mashahidi kwa wakati mmoja.

Nchimbi alidai sheria inataka ushahidi unapotolewa na shahidi mmoja,  mashahidi wengine wanaokusudia kutoa ushahidi katika kesi hiyo wasiwepo.

Alidai iwapo upande wa utetezi watapewa nafasi ya kusikiliza mashahidi kabla ya washtakiwa kujitetea, washtakiwa hawataruhusiwa kusikiliza kinachosemwa na mashahidi.

Alidai ushahidi unapotolewa ni lazima washtakiwa wawepo hivyo hawawezi kuwaondoa wakati wao ni sehemu ya shauri hilo.

Hata hivyo, aliomba mahakama itoe mwongozo utakaowataka washtakiwa hao kutoa utetezi wao kabla ya mashahidi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango aliiomba mahakama iendelee na utaratibu wa kawaida ambao umekubalika katika mahakama zote wa washtakiwa wanaanza kutoa ushahidi kabla ya mashahidi wengine.

"Tunaomba mheshimiwa usishawishike kuanza kitumia utaratibu uliojengeka katika kesi za uchaguzi na madai kwa sababu kesi za jinai zina utaratibu wake," alieleza Mango.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala baada ya kusikiliza hoja hizo za upande wa mashtaka alidai hakuna kifungu chochote cha sheria za hapa nchini au nchi za jirani ambazo zinazuia washtakiwa kusikiliza mashahidi  wake kwanza kabla ya washtakiwa mwenyewe.

Kibatala aliendelea kueleza mahakamani hapo kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachoeleza wakati shahidi anatoa ushahidi mashahidi wengine watoke nje ni kwa busara tu za mahakama.

Hata hivyo, Kibatala aliomba mahakama iwaruhusu kumuita shahidi ambaye wamemuandaa  kuwa wa kwanza na hii ni mara ya tatu anakwenda mahakamani hapo.

Aliongeza upande wa mashtaka wanajua namna ya kuendesha kesi yao na upande wa utetezi pia  wanajua jinsi ya kuendesha kesi yao.

Awali, Kibatala aliieleza mahakama kuwa washtakiwa hao watatoa ushahidi wao chini ya kiapo kwa kadri dini zao zinavyoruhusu.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kueleza kuwa katika kesi yao hiyo wataita mashahidi wengi na kwamba wanaye shahidi mmoja ambaye ataanza kutoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo.

Nchimbi alidai kuwa utaratibu wa mashahidi kuanza kutoa ushahidi washtakiwa watoe baadaye unakinzana  na miongozo ya kisheria na kwamba wanaupinga utaratibu huo.

Hata hivyo, Nchimbi aliongeza kuwa  utaratibu huo hauna misingi ya kisheria unayoiunga mkono.

Washtakiwa hao wanaanza kutoa utetezi wao baada ya mashahidi  nane wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na Mahakama kuwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu wajitetee.

Wanaokabiliwa katika kesi hiyo,  mbali Mbowe ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar-Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji.

Wengine ni wabunge; John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendajia jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.


Advertisement