Wanasiasa Kenya wapigwa marufuku kufanya siasa kanisani

Wednesday September 11 2019

Nairobi, Kenya. Kanisa Katoliki nchini Kenya limepiga marufuku wanasiasa wenye tabia ya kufanya siasa wawapo kanisani.

Zuio hilo limekuja siku chache baada ya wanasiasa mjini Kisumu kutwangana makonde walipokuwa wakihudhuria ibada Jumapili iliyopita.

Ugomvi huo ulihusisha mbunge Ndindi Nyoro na Maina Kamanda ambao wote wanatoka eneo la Kisumu waliokuwa wakihudhuria ibada katika kanisa la Gitui

Taarifa ya kanisa hilo iliyosainiwa na Askofu wa Dayosisi ya Murang’a, James Maria Wainaina ilisema kitendo kilichofanywa na wabunge hao ni aibu na hakipaswi kufumbiwa macho.

Askofu Wainaina alisema makasisi wote wameagizwa kufutilia mbali mialiko yote ya harambee kwa wanasiasa, akisema tukio la Jumapili limeaibisha kanisa hilo.

 “Wengi wenu mnafahamu kilichotokea katika parokia ya Gitui. Sisi sote tumeaibika ndiyo maana ningependa kuwajuza kwamba mfutilie mbali mialiko yote ya wanasiasa katika makanisa yenu,” ilisema sehemu ya tarifa hiyo.

Advertisement

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti la Taifa Leo, askofu huyo alisema “ingawa sijapata taarifa rasmi ya kanisa juu ya tukio hilo lakini ninataarifa ya kila kilichoendelea, ni lazima tuhakikishe kitendo hiki hakijirudii.

“Ni jambo la kusikitisha tukio hilo lilifanyika katika kanisa letu. Sikuwa na habari kwamba kulikuwa na wageni ambao walialikwa na nilisikia tu kupitia vyombo vya habari kuwa ghasia zilikuwa zimetokea. Nimeagiza uchunguzi ufanywe mara moja   kabla ya kuchukua hatua,” alisisitiza Askofu Wainaina.

Kauli ya askofu huyo inakuja baada ya Mkuu wa kanisa hilo nchini Kenya, Kadinali John Njue kuwaachia maaskofu wa parokia mbalimbali jukumu la kufanya maamuzi ili kuamua iwapo viongozi wanaohudhuria ibada kwenye maeneo yao, wataruhusiwa kuwahutubia waumini au la kama njia ya kuzuia ghasia kati ya wanasiasa wa mirengo mbalimbali.

Kadinali Njue alisema ni maaskofu ndiyo wanaelewa hali ya kisiasa katika parokia wanazosimamia kwa hivyo wao ndio wanafahamu njia ya kukabiliana na joto la kisiasa linalozidi kupanda kwenye maeneo hayo.

 “Maaskofu wanafaa kutoa ushauri ili kuepuka aibu inayosababishwa na vurugu kwenye makanisa yetu. Hii ni kwa sababu wao ndio wanaelewa parokia zao na wanafaa kutoa uamuzi wa mwisho,” alisema Kadinali Njue kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Advertisement