Wanasoka nyota watano watakaotikisa Italia 2019/20

Muktasari:

Ligi Kuu ya Italia inaanza kesho Jumamosi huku Juventus ikianza harakati za kusaka ubingwa kwa msimu wa tisa mfululizo.


Juventus, ambao wamekuwa wakishikilia ubingwa wa soka wa Italia kwa misimu minane, wanaanza kampeni ya kutetea taji lao na Napoli watakuwa wakiwania kombe hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 wakati Ligi Kuu ya Soka ya Italia (Serie A) itakapoanza mwishoni mwa wiki hii.

Juventus, ikiwa bila ya kocha mpya Maurizio Sarri, inakwenda kuvaana na Parma kesho Jumamosi, ikiwa imeongezwa nguvu kutokana na kuwasili kwa Matthijs De Ligt, Aaron Ramsey na Adrien Rabiot pamoja na kipa mkongwe Gianluigi Buffon aliyerejea Turin.

Napoli, inayofundishwa na Carlo Ancelotti itaenda kuvaana na Fiorentina, huku timu hiyo ya Tuscany ikiwa imeimarika baada ya kumsajili mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Franck Ribery aliyeondoka Bayern Munich akiwa huru.

Inter Milan, ambayo inamilikiwa na Mchina, pia ilimwaga fedha kuimarisha kikosi cha kocha Antonio Conte ambaye atakuwa akikifundisha kwa mara ya kwanza, kw akumsajili Romelu Lukaku aliyenunuliwa kwa dola 72 milioni za Kimarekani.

AFP Sport inaangazia wachezaji muhimu watano wanaoweza kung'aa:

- Cristiano Ronaldo (Juventus) -

Mshambuliaji nyota Mreno, Christiano Ronaldo anaanza msimu wa pili jijini Turin baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kubwa katika nchi ya tatu barani Ulaya msimu uliopita. Ronaldo, ambaye ameshinda tuzo ya Mpira wa Dhahabu mara tano, anatarajiwa kuwa kiongozi wa timu hiyo iliyo katika kipindi cha mpito baada ya kuondoka kwa Massimiliano Allegri. Ronaldo, 34, alilazimika kusubiri hadi mechi ya nne ya ligi msimu uliopita ili aanze kuichezea Juventus, lakini akafunga mabao 28 katika mechi 43 - 21 katika ligi ya Serie A, sita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja katika mechi ya Super Cup. Idadi hiyo ni ndogo kuliko zote kwake katika kipindi cha muongo mmoja na ndiyo itakuwa kichochea cha kutaka afanye vizuri ili ashinde taji la Ulaya.

 

- Matthijs De Ligt (Juventus)

Matthijs De Ligt ni mmoja kati ya wachezaji wanaosakwa sana barani Ulaya. Beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 19 alikuwa nahodha wa Ajax iliyofanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita, ikiziondoa Real Madrid na Juventus na kufika nusu fainali huku ikitwaa mataji mawili ya Uholanzi.

Lakini nyota huyo alisema nafasi ya kucheza pamoja na Ronaldo haikuwa ya kuipoteza. Nyota huyo chipukizi amekuwa mchezaji muhimu katika ngome ya Juventus akicheza pamoja na wakongwe Giorgio Chiellini, 35, na Leonardo Bonucci, 32.

- Romelu Lukaku (Inter Milan)

Romelo Lukaku hakufurahia kuondoka Manchester United lakini mshambuliaji huyo mwenye nguvu amekuwa nyota baada ya kununuliwa na kocha wake wa zamani katika klabu ya Chelsea, Antonio Conte, ambaye alijaribu bila mafanikio kumnyakua mshambuliaji huyo mwaka 2017 kabla ya kuhamia Old Trafford akitokea Everton. Mshambuliaji huyo mwenye miaka 26 na anayeongoza kwa ufungaji katika historia ya timu ya taifa ya Ubelgiji, atakuwa kinara wa safu ya ushambuliaji ya Inter, akichukua jezi namba 9 kutoka kwa nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Mauro Icard. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea na West Bromwich amekasirishwa na madai kuwa bado hajawa katika hali nzuri kimchezo kuweza kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Lecce ambayo imepanda daraja msimu huu.

"Si kitu kizuri kwa kijana mnene," aliandika katika akaunti yake ya Instagram akionyesha kutoridhishwa na madai hayo.

- Hirving Lozano (Napoli)

Hirving Lozano, mchezaji wa kimataifa wa Mexico amefanya vizuri misimu miwili iliyopita akiwa na PSV Eindhoven akifunga mabao kutokea pembeni. Akijulikana kwa kasi yake, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alijiunga na PSV akitokea Pachuca mwaka 2017 na muda mfupi baadaye akawa tishio katika soka la Uholanzi. Winga huyo ambaye amepachikwa jina la 'Chucky' amefunga mabao 45 katika mechi 83 katika kipindi cha misimu miwili. Anatarajia kukamilisha uhamisho wake wa thamani ya euro 42 milioni.

- Mario Balotelli (Brescia)

Mario Balotelli huchukuliwa kama "mtoto mbaya" lakini amepania kuonyesha makali yake katika klabu ya mtaani kwao ya Brescia wakati akiwania kuwepo katika kikosi cha Italia kitakachoshiriki fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2020. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, ameshaichezea Italia mechi 36 na mara ya mwisho kucheza Serie A alikuwa AC Milan aliyoichezea kwa mkopo akitokea Liverpool msimu wa mwaka 2015-2016. Balotelli amekuwa akirushiwa maneno ya kibaguzi na mashabiki nchini Italia. "Natarajia, kutoka moyoni, kupata ligi to0fauti na si vitendo tofauti vipya vya kibaguzi," alisema. Kwanza, atalazimika kumalizia adhabu ya kutocheza mechi nne baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu wakati akiichezea Marseille kabla ya kucheza mechi ya kwanza Septemba 25 dhidi ya Juventus.