Wanaume tegemezi ni watatu Zaidi ya wanawake

Muktasari:

Wakati uwiano wa wanawake wanaoongoza kaya ukiongezeka, imebainika kuwa viwango vya wanawake kuwa tegemezi ni chini ya vile vya wanaume.

Wakati uwiano wa wanawake wanaoongoza kaya ukiongezeka, imebainika kuwa viwango vya wanawake kuwa tegemezi ni chini ya vile vya wanaume.

Kwa mujibu wa utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (HBS) wa mwaka 2017/18 unaotolewa na Ofisi  ya Taifa ya Takwimu (NBS), katika kila watu 100, wanaume tegemezi ni watatu zaidi ya wanawake.

Utafiti huo unaonyesha kuwa wastani wa wanawake tegemezi ulikuwa 46 katika kila wanawake 100 wakati wanaume tegemezi wakiwa takribani 49 katika kila wanaume 100. Hiyo ina maana kuwa katika watu 100 tegemezi nchini wanaume tegemezi ni watatu zaidi ya wanawake.

Akifafanua maana yake, Sylvia Meku wa NBS alisema utegemezi huo ni ule wa mahitaji maalumu, yaani chakula, mavazi na malazi.

“Ripoti inazungumzia watu tegemezi ambao wanategemea mahitaji muhimu,” alisema.

Mtaalamu huyo alieleza kuwa watu tegemezi waliolengwa zaidi ni watoto wa chini ya miaka 15 na wazee wa miaka 65 au zaidi.

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Rose Reuben alisema matokeo ya ripoti hiyo yanadhirisha hali iliyopo kwenye jamii zetu kwa kuwa wanawake wanajishughulisha na hawachagui kazi.

“Wanawake wanafanya shughuli ndogondogo, hutegemei kuwakuta wanaume wanafagia barabara lakini wanawake wapo wengi ndio maana si tegemezi. Lakini hii haimaanishi kuwa wana vipato vikubwa isipokua ni vile vinavyowafanya wasiwe tegemezi,” alisema Ruben.

Mkurugenzi huyo wa Tamwa alieleza kuwa kwa ongezeko hilo la idadi ya wanawake ambao ni viongozi wa kaya lina ishara nyingi na miongoni mwa hizo ni uwezekano kuwa wajane au wametelekezwa lakini pia maana kubwa ni kuwa sasa wanawake wameweza kuinuka na hivyo kampeni za wanawake wanaweza zimefanya kazi.

Naye Josephine Tesha, mwanasaikolojia kutoka MNH, alisema katika suala la utegemezi tunatizama zaidi uhalisia wa tabia kati ya wanaume na wanawake.

“Kisaikolojia tukimaanisha saikolojia inalenga hasa akili ya mwanadamu na jinsi inavyofanya kazi. Pamoja na kwamba kimwili wanaume wana nguvu kuliko wanawake, lakini kiakili kuhimili changamoto za maisha na kifikra, wanawake wana nguvu na uwezo mkubwa wa kuhimili hali yoyote ya maisha zaidi ya wanaume,” alisema.

 “Wanawake wana uwezo wa kutumia akili zao kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kuliko wanaume (mult tasking). Ni wazi kabisa kutokana na hali ya kiuchumi kwa sasa imefanya wanawake kuhimili na kukabiliana na changamoto kuliko wanaume kwa sababu ya uwezo wa wanawake kisaikolojia.”

 Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa kaya zinazoongozwa na wanawake zilikuwa asilimia 27.4 mwaka 2017/18, ikiwa ni wastani wa juu kidogo ikilinganishwa na asilimia 24.7 ya kaya zilizokuwa zikiongozwa na wanawake mwaka 2011/12 na mwaka 2007.

Mkurugenzi huyo wa Tamwa alieleza kuwa kuongezeka kwa wanawake wanaoongoza kaya kunaendana na kupungua kwa wanawake tegemezi na kwamba jamii bado inahitaji kuamka hasa vijana.

“Wakati umefika sasa kwa wanaume kutodharau kazi na kuwa wajasiri hata kwa kuanza na shughuli ndogo kwani hata hao waliofanikiwa walianza taratibu,”  alisema.

 “Licha ya kuwapo na changamoto za mifumo ya elimu ambayo haiwaandai watu kujitegemea zaidi ya kuwa tegemezi, vijana wanatakiwa wajiamini na kuanza hata kidogo kidogo.

Kwa upande wake, Josephine alitaka watu wengi kujitokeza katika kutafuta msaada wa kisaikolojia kwa changamoto zozote wanazokutana nazo, kwa kuwa ni kwa kukutana na mwanasaikolojia wanaweza kupata uelewa mzuri zaidi na kujielewa kuhusu fikra zao pamoja na namna ya kukabili changamoto zilizoko mbele yao.

“Hata kama uwezo wa kutafuta msaada wa kisaikolojia huna jenga tabia ya kuongelea fikra zako kwa watu ambao wanaweza kukusikiliza,  kwani kuongelea fikra zako ni hatua ya kwanza katika kuzitatua, ” alieleza

Takwimu zaidi

Vile vile matokeo ya HBS yanaonyesha kuwa umaskini una uhusiano na jinsi ya mkuu wa kaya. Asilimia 26.1 ya kaya zinazoongozwa na wanaume na asilimia 27.4 ya kaya zinazoongozwa na wanawake ni maskini kwa kigezo cha umaskini wa mahitaji ya msingi unaojumuisha chakula.

Vile vile, asilimia 8.1 ya kaya zinazoongozwa na mwanaume na asilimia 7.9 zinazoongozwa na mwanamke ni maskini wa chakula.

Wastani wa ukubwa wa kaya za Tanzania Bara ni watu 4.6.  Kaya zinazoongozwa na wanaume watu wanne mpaka watano zina wanakaya wengi kuliko kaya zinazoongozwa na wanawake zina wastani wa watu wanne.

Uwiano wa wanakaya tegemezi katika ngazi ya taifa takribani nusu ya watu nchini ni tegemezi sawa na wastani wa asilimia 47.8.

Hali ikiwa  mbaya zaidi vijijini, ambapo zaidi ya nusu (asilimia 51.3) ya idadi ya watu ni tegemezi ukilinganisha na asilimia 40.4 katika maeneo ya mijini.

Utegemezi unatofautiana kimkoa ambapo Mkoa wa Simiyu (asilimia 55.2) una uwiano mkubwa zaidi wa tegemezi na Dar es Salaam (asilimia 35.0) una uwiano mdogo zaidi.