Wanaume wanaopigwa, kutelekezwa na wake zao watakiwa kutoa taarifa

Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera akizungumzia hatua zilizochukuliwa na mkoa  kukabiliana na ukatili wa kijinsia. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

Wanaume Mkoa wa Katavi nchini Tanzania ambao wanaigwa na wake zao na kutelekezwa wametakiwa kutoona aibu, watoe taarifa ili changamoto zinazowakabili zipatiwe ufumbuzi.

Katavi. Wanaume Mkoa wa Katavi nchini Tanzania ambao wanaigwa na wake zao na kutelekezwa wametakiwa kutoona aibu, watoe taarifa ili changamoto zinazowakabili zipatiwe ufumbuzi.

Hayo yameelezwa jana Jumatatu Februari 24, 2020 na mkuu wa Mkoa wa Katavi,  Juma Homera katika  uzinduzi wa msafara wa kitaifa wa kupinga ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na idara kuu ya maendeleo ya jamii, kuelekea maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wanawake duniani.

"Kutelekezwa hakuna mwenyewe hata mimi naweza kuachwa, lakini  wapo wanaume wanapigwa hawasemi wanaona aibu. Wajitokeze  waeleze namna wanavyopigwa, waseme ili vyombo vya dola tuchukue hatua  kwa mujibu wa sheria," amesema Homera.

Homera amesema katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia Mkoa huo kwa kushirikiana na wizara husika wametatua kesi za kutelekezwa zaidi ya 314,  za watoto ni 100, wanawake  100 na  14  za wanaume.

Mmoja wa washiriki, Juma Hassan mkazi wa Mpanda amekiri baadhi ya wanaume kupigwa na kutelekezwa bila kufahamu kuwa wana haki ya kutoa taarifa.

Mwakilishi wa Katibu mkuu wa Idara  kuu ya maendeleo ya jamii,  Imelda Kamugisha amesema lengo la msafara huo ni kusaidia kuendeleza mapambano ya kutokomeza vitendo vya kikatili nchini ambavyo vimekithiri katika jamii.

"Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokomea kwa kasi na tumeamua kuanzia Katavi kutokana na takwimu kuonyesha kuna tatizo ni kubwa," amesema Imelda.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii walioambatana na msafara huo Nurdin Bilal maarufu  Shetta amesema ili kufanikisha adhima ya serikali ya  kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia jamii inatakiwa kushirikiana kufichua na kutoa taarifa sehemu husika.

"Tuwalinde watoto, tunatumia Sanaa kufikisha ujumbe katika jamii  kupinga vitendo vya ukatili, tusiwe chanzo cha tatizo," amesema Shetta.

Msafara huo pia utaifikia mikoa ya Rukwa, Songwe, Njombe, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga na Simiyu ambayo inatajwa kuathirika zaidi na tatizo hilo.

Kauli mbiu ni 'Tokomeza ukatili wa kijinsia twende pamoja'.