Wanawake, vijana Kinondoni watengewa Sh3.4 bilioni

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo.

Muktasari:

Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imetenga  Sh3.4 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu katika bajeti ya mwaka 2020/21.

Dar es Salaam. Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imetenga  Sh3.4 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na wenye ulemavu katika bajeti ya mwaka 2020/21.

Akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo leo Jumanne Februari 25, 2020 mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo amesema fedha hiyo itatokana na mapato ya ndani.

Amebainisha kuwa Sh1.3 bilioni itatolewa kwa wanawake, Sh1.3 bilioni  kwa vijana na Sh690.4 milioni kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Na tumeweka mkakati wa kuhakikisha makundi haya yanapatiwa pesa kwa wakati na bila kero yoyote,” amesema Chongolo.

Akizungumzia mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye wilaya hiyo, Chongolo amesema wanatarajia kujenga kituo cha daladala katika eneo la Mwenge.

“Kituo hicho pia kitazungukwa na maduka mbalimbali lakini pia tutajenga uwanja wa mpira kwenye eneo hilo,” amesema Chongolo.

Mbunge wa Kinondoni (CM), Maulid Mtulia aliishauri kikao hicho kutafuta takwimu za watu wenye ulemavu ili waweze kusaidiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema hoja ya kuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu ni muhimu kwa sababu itasaidia kundi hilo kufikishiwa mahitaji muhimu ikiwamo mikopo.

“Hata hili suala la kuwaunganisha kwenye vikundi vya uchumi naona kama linawagawa kwamba walemavu watafutane, wakae pamoja ndio wapewe mikopo. Nadhani pamoja na hilo, walemavu wachanganywe kwenye makundi,” amesema Makonda.