Wanawake ACT-Wazalendo watoa neno uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

  • Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT- Wazalendo imemuomba Rais wa Tanzania,  John Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kusaka maridhiano kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT- Wazalendo imemuomba Rais wa Tanzania,  John Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kusaka maridhiano kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Pia, wamemuomba kiongozi mkuu huyo wa nchi kukutana na viongozi wa Serikali kuangalia dosari zilizojitokeza wakati wagombea wakichukua na kurejesha fomu na kusababisha vyama saba kujitoa katika uchaguzi huo.

“Tunamuomba Rais wetu kwa heshima  aingilie kati, asikae kimya ameingilia mambo mengi na yamefanikiwa  tuna imani na hili la uchaguzi ataliona.”

“Tunamuomba akae na viongozi wa vyama kusikiliza maombi yao kwa maslahi ya Watanzania,” amesema Chiku Abwao, mwenyekiti wa Ngome ya chama hicho.

Amesema Magufuli kukaa kimya katika suala hilo kunatia dosari uongozi wake na ataacha historia mbaya muda wake ukimalizika.

“Tunataka haki na sheria izingatiwe na sio kila siku kusikia matamko, demokrasia itumike na hii sio kwa vyama vya upinzani bali kwa maslahi ya nchi yetu, hatutaki baadaye nchi itumbukie kwenye machafuko tunataka amani irejee kama ilivyokuwa mwanzo,” amasema Chiku.

Vyama vilivyotangaza kutoshiriki uchaguzi huo ni ACT- Wazalendo, Chadema, UPDP, Chauma, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

Vyama hivyo vimejitoa kwa madai ya kutotendewa haki kutokana na wagombea wake kuenguliwa bila sababu za msingi. Hata hivyo Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo ameagiza waliochukua fomu na kuzirejesha kupitishwa kugombea.