Wanawake watano ‘wanaojiuza’, mteja wao wahukumiwa kwenda jela

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limewakata na kuwafikisha mahakamani wanawake watano na mwanaume mmoja aliyekuwa akimnunua mmoja wao kuhukumiwa kifungo jela.


 


Dodoma. Jeshi la Polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limewakata na kuwafikisha mahakamani wanawake watano na mwanaume mmoja aliyekuwa akimnunua mmoja wao na wote kuhukumiwa kifungo jela.

Wakati watano wakihukumiwa kifungo cha miezi sita, mmoja amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu baada ya kukiri kosa.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 11, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema watu hao walikamatwa Septemba 8, 2019 katika operesheni zinazofanywa na polisi maeneo mbalimbali mjini Dodoma.

Kamanda Muroto  amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu 176 (a) (f) (g) cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Amesema usiku katika mtaa wa Uhindini  na Viwandani, waliwakamatwa wanawake watano wakifanya biashara ya ukahaba huku wakidaiwa kuhatarisha amani na utulivu katika mtaa huo.

Amebainisha kuwa mwanamke mmoja kati yao alikamatwa akifanya ngono na mwanaume huyo, wote wamehukumiwa kifungo  na kuchapwa viboko vitatu kila mmoja.

Amewataka watu hao kuwa ni Erica George (24) mkazi wa Mailimbili;  Lucy Saibati (28) mkazi wa Bahi Road;  Joyce Ndekwa (30) mkazi wa Veyula;  Hawa Said (28) mkazi wa Airport  na Glory Michael (29) mkazi wa Mailimbili  na  Pascal George (28) mkazi wa Nzuguni.

Septemba 5, 2019 Muroto aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi iliwafikisha mahakamani wanawake 15 na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kila moja baada ya kupatikana na hatia ya kujiuza.

Alieleza kuwa ulifanyika msako Septemba 2, 2019 saa tatu usiku mtaa wa Uhindini na kuwakamatwa wanawake 15 wakifanya biashara ya ukahaba huku wakidaiwa kuhatarisha amani na utulivu katika mtaa huo.

Alisema wamepelekwa gereza la Isanga na kupokewa kwa ajili ya nguvu kazi, kwamba wataponda kokoto na kufanya kazi nyingine.

Aliwataja kuwa ni  Suzana Onesmo (27), Mariam Omary (29), Maimuna Issa (38), Bhoke Chacha (30), Swaumu Bakari (26),  Rahma Abdi (28), Magreth Humphrey (27),  Wema Saidi (25),  Jeniffer Wilson (33), Lydia Kilale (30),  Manka Richard (21),  Mwasuma Hassan (26),  Angel Joseph (29), Zaina ramadhani (30) na Tatu Saidi (27).”