Wanyamapori waliopo maeneo ya mijini nchini Tanzania kupigwa mnada

Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla

Muktasari:

Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla amesema Serikali itauza viboko wote waliopo kwenye maziwa, mabwawa na mito yaliyopo maeneo ya mijini.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla amesema Serikali itauza viboko wote waliopo kwenye maziwa, mabwawa na mito yaliyopo maeneo ya mijini.

Kigwangalla ametaja miongoni mwa maeneo ambayo yana viboko watakaouzwa ni Mpanda, Mafia, Babati na kwamba mauzo hayo yatafanyika kwa  mnada kwa utaratibu ambao utatangazwa wiki ijayo

Kigwangalla amesema mbali na viboko pia Serikali imeamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini kutokana na kujitokeza changamoto mpya.

“Uhifadhi na ulinzi wa maliasili nchini umeimarika na tumepata mafanikio. Ujangili tumeudhibiti kwa mafanikio makubwa sana. Changamoto mpya imezaliwa, wanyama wakali waharibifu wamezidi na wanavamia maeneo ya watu,” amesema Dk Kigwangalla.

Katika taarifa aliyotoa kupitia akaunti yake ya Twitter imeeleza kuwa pia wanaanzisha mradi wa kuweka uzio kwenye maeneo yenye historia ya matukio ya mamba kudhuru watu, kama Maleza na Ruvu.

“Tunawaomba wananchi wasifanye mauaji ya kulipiza kisasi tukitekeleza haya, pia waache tabia hatarishi” amesema Kigwangalla.

Mbunge huyo wa Nzega Vijijini (CCM) amesema wanaanzisha vituo vya kudumu vya ulinzi kwenye maeneo korofi, ambako  wanyama wakali na waharibifu wamekuwa wakileta shida kwa wananchi.

Waziri huyo ametaja sababu ya kufanya maamuzi hayo ni kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori ambayo imeibuka baada ya kukamilika kwa utafiti alioagiza ufanywe na taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (Tawiri) Julai 2018 alipofanya ziara ya ‘Pori kwa Pori’ kutembelea ziwa Rukwa.