Wapigwa faini ya Sh230 milioni baada ya kusafirisha makontena 18 ya magogo, bila kibali

Thursday March 26 2020

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu raia wawili wa India, Manish Khattar(38)na Rajesh Velram(52)  kulipa faini ya Sh230 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na makontena 18 ya magogo aina ya mpigo yenye thamani ya Sh500 milioni.

Pia, mahakama hiyo imetaifisha magogo hayo na kuwa mali ya Serikali.

Mbali na adhabu hiyo, washtakiwa hao wamehukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja, kwa kutokujihusisha na kosa lolote la jinai katika kipindi cha muda huo.

Khattar na Velram, wote wakazi wa Upanga na Wakurugenzi wa Kampuni ya Best Ocean Air Limited and Freight Exchange Ltd, wanadawa kusafirisha magogo hayo kutoka Zambia kuelekea China.

Washtakiwa hao wametiwa hatiani katika shtaka moja la kukutwa na magogo, baada ya kukiri mashtaka yao na kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania(DPP).

Akisoma hukumu hiyo leo, Machi 26, 2020, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega amesema washtakiwa wametiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na mazao ya misitu, ambayo ni magogo, kinyume cha sheria.

"Mmetiwa hatiani kama mlivyoshtakiwa, hivyo kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh115 milioni kila mmoja, pia magogo yaliyokamatwa yatataifishwa na kuwa mali ya Serikali,”amesema hakimu Mtega.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini hiyo na kuachiwa huru na mahakama.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude akisaidiana na Maternus Marandu na Ladslaus Komanya, alidai kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali, baada ya kufanya majadiliano na DDP kuhusu kukiri mashtaka yao na kupunguziwa adhabu.

Hata hivyo, kabla mahakama kutoa adhabu hiyo jopo la mawakili watatu wa upande wa utetezi likiongozwa na Shabani Mlembe akisaidiana na Lightness Minja na Alfredy Affa aliiomba mahakama kuwapatia wateja wao adhabu nafuu kwa kuwa bado wanategemewa na wana familia zao na ni kosa lao la kwanza.

“Tunaiomba mahakama iwapatie wateja wetu adhabu nafuu kwa sababu kwanza, hawajaisumbua mahakama lakini pia wanategemewa na familia hivyo tunaomba mahamaka izingatie maombi yetu”aliomba wakili Mlembe.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo , Januari 29, 2020 wakikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kukwepa kodi, kusafirisha magogo na kutakatisha fedha, lakini baada ya kufanya mazungumzo na DDP, washtakiwa hao walifutiwa mashtaka sita na kubakishiwa shtaka moja ambalo ni kusafirishwa mazao ya misitu bila kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS).

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa lao, kati ya Januari 15, 2015 na Oktoba 31, 2015 katika eneo la NASACO, lililopo Temeke.

Inadaiwa kuwa wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Best Ocean Air Limited and Freight Exchange Ltd, wanadawa kusafirisha magogo aina ya mpingo yakiwa katika makontena 18 yakitokea Zambia kuelekea China, kupitia Tanzania, yenye thamani ya Sh 505milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS).

Advertisement