Wapinzani Tanzania wahoji bajeti uendeshaji wa mapori yaliyopandishwa hadhi
Muktasari:
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni nchini Tanzania imemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii nchini, Dk Hamis Kigwangala kulieleza Bunge ni fungu gani limeridhiwa na chombo hicho cha kutunga sheria kwa ajili ya uendeshaji wa Hifadhi za Kigosi na Ugalla.
Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni nchini Tanzania imemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii nchini, Dk Hamis Kigwangala kulieleza Bunge ni fungu gani limeridhiwa na chombo hicho cha kutunga sheria kwa ajili ya uendeshaji wa Hifadhi za Kigosi na Ugalla.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Septemba 10, 2019 na mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Catherine Ruge kwa niaba ya msemaji wa kambi hiyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ruge alikuwa akisoma maoni ya kambi hiyo kuhusu Azimio la kuridhia mapendekezo ya ubadilishaji hadhi sehemu ya pori la akiba la Ugalla kuwa hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla na eneo la pori la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi.
Akisoma maoni hayo, Catherine amesema uamuzi huo unatolewa bila kuwepo kwa kasma ya uendeshaji, kwamba si kama unalisaidia Taifa kwani analazimika kunyang’anya fedha ambazo tayari zimeshapangiwa matumizi kwenye bajeti na kusababisha miradi mingine kusimama hadi uamuzi wa dharura utekelezwe.
“Ikumbukwe kuwa muda ni raslimali pindi unapopita haurudi tena na hiyo ni hasara ambayo haiwezi kufidiwa,” amesema.