Wapinzani Tanzania wahoji fedha za maendeleo ya kilimo kutolewa kidogo

Waziri Kivuli wa Kilimo, Pascal Haonga akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuz

Muktasari:

  • Waziri Kivuli wa Kilimo nchini Tanzania, Pascal Haonga amesema bajeti ya maendeleo katika sekta ya kilimo hairidhishi, kwa miaka mitatu mfululizo imetolewa kidogo.

Dodoma. Waziri Kivuli wa Kilimo nchini Tanzania, Pascal Haonga amesema bajeti ya maendeleo katika sekta ya kilimo hairidhishi, kwa miaka mitatu mfululizo imetolewa kidogo.

Akizungumza  bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Februari 5, 2020, Haonga ambaye pia ni mbunge wa Mbozi (Chadema) amesema utekelezaji wa bajeti unasuasua ikiwa imepita imeshapita nusu ya mwaka.

Amesema mwaka 2019/2020 bajeti iliyotengwa kwa ajili ya maendeleo katika kilimo ilikuwa ni Sh143.5bilioni lakini zilizotolewa hadi sasa ni Sh21.4bilioni.

Amesema licha ya fedha hizo kutolewa kidogo kiwango kinachotoka kwa wafadhili ni kikubwa kuliko kinachotolewa na Serikali.

“Utekelezaji umekuwa wa tabu sana na wa  kusuasua. Hali ni mbaya,” amesema Haonga.

Ameitaka Serikali kulipa madeni yanayodaiwa na wakulima wa pamba na korosho nchini ili kuwawezesha kuendeleza kilimo nchini.

Amesema mbolea aina ya Urea haipatikani katika maeneo mbalimbali nchini wakati ndio msimu wa kilimo.

Amesema bei elekezi ya mbolea hiyo ni Sh54,000 lakini hivi sasa inauzwa kati ya Sh64,000 hadi Sh70,000.