Wapinzani waiongezea CCM ruzuku ya Sh1.1 bilioni

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania (CCM) kimejivunia ongezeko la ruzuku kutoka Sh12.4 bilioni kwa mwaka 2015/16 hadi Sh13.5 bilioni kwa mwaka baada ya wabunge na madiwani wa upinzani kuhamia katika chama hicho.

Mwanza. Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania (CCM) kimejivunia ongezeko la ruzuku kutoka Sh12.4 bilioni kwa mwaka 2015/16 hadi Sh13.5 bilioni kwa mwaka baada ya wabunge na madiwani wa upinzani kuhamia katika chama hicho.

Akifungua mkutano wa majadiliano ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) jijini Mwanza leo Alhamisi Desemba 12, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema wapinzani kuhamia CCM ni ishara na uthibitisho wa uimara, utendaji na uongozi bora ndani ya chama na Serikali.

“Jambo jingine la kujivunia na kufurahisha zaidi ni kwamba katika miaka minne iliyopita chama chetu kimeendelea kupokea wanachama mbalimbali kutoka vyama vya upinzani, wakiwemo Wabunge na Madiwani. Hii imepelekea ruzuku kuongezeka kutoka Sh 12.4 kwa mwaka 2015/16 hadi Sh13.5 bilioni kwa mwaka, hivi sasa,” amesema Rais Magufuli.

Chadema na CUF ni miongoni mwa vyama vya siasa ambavyo wabunge na madiwani wake walihamia CCM, kupitishwa kuwania nafasi hizo na kushinda.

Wabunge wa Chadema waliohamia CCM  ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Marwa Ryoba (Serengeti), Godwin Molell (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati) na Joseph Mkundi (Ukerewe) huku CUF ikiwapoteza Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Kachauka (Liwale). 

Mwenyekiti huyo wa CCM amesema tangu achukue kijiti cha uongozi ametekeleza mikakati ya kuhakiki, kurejesha na kudhibiti mali za chama zilizokuwa mikononi au kutumiwa na watu binafsi.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema uhakiki, kurejesha na udhibiti wa mali za chama unalenga kukifanya chama hicho kikongwe nchini kuondokana na utegemezi wa matajiri waliojifanya kuwa wafadhili na kujipa nguvu na mamlaka makubwa ya kimaamuzi ndani ya CCM.

“Tumefanya mageuzi ndani ya CCM kwa lengo la kuwa na chama imara na hatimaye Serikali imara, haiwezekani kuwa na Serikali imara inayoongozwa na chama dhaifu kwani hiyo inaweza kusababisha mtanziko wa kiuongozi,” amesema

Ametaja kupunguza idadi ya wajumbe wa NEC kutoka 342 hadi 168, kuwaondoa Makatibu wa mikoa kutoka miongoni mwa wajumbe wa NEC, kufuta nafasi za makatibu wasaidizi wa wilaya na mikoa na wale wa uchumi kuwa ni kati ya mikakati iliyoimarisha maamuzi na utendaji ndani ya CCM.