Wapinzani wataja chanzo cha hofu ya CCM uchaguzi mkuu

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli akifungua kikao cha Viongozi wa Mikoa na Wilaya, Watendaji wa Chama na Jumuiya zake wa kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam jana. Picha na Ikulu

Unaweza kujiuliza hofu ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu inatokana na nini? Kwa miaka minne imefanya siasa maeneo mbalimbali nchini, huku vyama vya upinzani vikilalamika kuikosa fursa hiyo.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2015, Serikali ilitangaza kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano isipokuwa katika maeneo ya wabunge na madiwani.

Uamuzi huo kwa kiasi kikubwa umeviathiri vyama vya upinzani ambako baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamejikuta wakipata misukosuko ikiwamo kukamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani.

Pamoja na yote hayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli ameonyesha kuvihofia vyama vya upinzani.

Akizungumza na watendaji wa chama na jumuiya zake za mikoa na wilaya hivi karibuni, Rais Magufuli alisema upinzani umebadilika, una mbinu za wazi na za siri za ushindi, hivyo wanaCCM wasibweteke hata kama chama hicho tawala kilipata ushindi wa asilimia 99 katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo ikiwa imepita takriban miaka minne baada ya mchuano mkali na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu 2015 ambako vilipata kura nyingi za urais pamoja na idadi kubwa ya wabunge na madiwani.

Katika uchaguzi huo, Magufuli alipata kura milioni 8.8, huku mgombea wa upinzani, Edward Lowassa aliyeungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akipata kura milioni 6.07.

Yaliyotokea baada ya uchaguzi 2015

Baada ya Rais Magufuli kuingia Ikulu, alipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano mpaka mwaka 2020 na kutaka watu waachwe wafanye kazi na kulijenga taifa na wanasiasa wasubiri kampeni za uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, katazo hilo lilipingwa na Chadema ambacho kilitangaza kufanya maandamano nchi nzima mwaka 2016 kupinga agizo hilo, hatua ambayo haikufanikiwa.

Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kukamatwa na kufikishwa mahakamani wakidaiwa kukaidi agizo hilo.

Pia ilishuhudiwa idadi kubwa ya madiwani na baadhi ya wabunge wa upinzani wakihama vyama vyao na kujiunga na CCM wakieleza kuwa wanaenda

‘kuunga mkono juhudi’ za Rais Magufuli kutokana na kufanikiwa katika maeneo mbalimbali.

Wabunge wa upinzani waliojiuzulu nafasi zao na wengine kufanikiwa kuzitetea kwa tiketi ya CCM ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Marwa Ryoba (Serengeti), Godwin Moleli (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati) na Joseph Mkundi (Ukerewe) ambao walikuwa Chadema, huku wale waliotoka CUF ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Zuberi Kachauka (Liwale) na Abdallah Mtolea (Temeke) .

Baadhi yao walidai wamefikia uamuzi huo kutokana na utendaji kazi wa Rais Magufuli, hivyo vyama vya upinzani havina hoja kwa kuwa mambo mengi waliyokuwa wakiyalalamikia yamefanyiwa kazi.

Hata mwaka jana wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vyama vinane vya upinzani vya Chadema, UMD, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo, CUF na Chauma vilisusa kushiriki uchaguzi huo kwa kile walichoeleza kufanyiwa figisu na wagombea wao wengi kuenguliwa.

Hali hiyo ilisababisha asilimia kubwa ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa na baadaye CCM ilitangaza kushinda kwa asilimia 99.

Siri vyama kuimarika

Pamoja na kupigwa kitanzi kwa miaka minne kutofanya siasa, vyama vya upinzani havikubweteka na badala yake vilibuni mbinu mbadala na kueleza mbinu hizo zimewasaidia kuimarika.

Vyama hivyo vilifanya siasa za moja kwa moja za kuwafikia wananchi vijijini pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kujiimarisha. Hali hiyo inadaiwa kuwasaidia kuvutia wafuasi wengi na pia kupata idadi kubwa ya wanachama.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema pamoja na mazingira magumu ya kufanya siasa, chama hicho kimebuni njia mbadala na kufanikiwa kujiimarisha zaidi.

Alisema wamejenga chama katika mitaa, vijiji na vitongoji. Katika vitongoji 64,416 wamefika kwenye vitongoji zaidi ya 60,000 na kuandikisha wanachama pamoja na kuwa na viongozi.

Mbowe alisema kwa sasa anatamani zaidi siasa za namba, kwani hata wakati wa kugombea uhuru wa nchi hakukufanyika mikutano ya hadhara.

“Mbinu zile zile za mababu zetu walizotumia za mguu kwa mguu, nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda tunakwenda kuziimarisha,” alisema na kuongeza kuwa sasa wanajivunia kuwa na wanachama zaidi ya milioni sita nchini.

Kauli za wanasiasa

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika anasema hofu ya CCM inatokana na ukweli kwamba vyama vya upinzani vimejiimarisha, licha ya kuzuiwa kufanya siasa kwa miaka minne.

Anasema baada ya zuio hilo hawakubweteka, bali walitumia mbinu za chini kwa chini kufanya siasa katika vijiji, vitongoji na kata kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja.

“Chadema imetusaidia sana kujiimarisha. Walijua kwa kuzuia mikutano ya hadhara vyama vitadhoofika, hata katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana baada ya kugundua nguvu ya upinzani walitufanyia figisu.

“Tulisimamisha wagombea kila eneo ambao walitokana na matakwa ya wananchi bada ya kura za maoni ndani ya chama, walipoona hali hiyo na kubaini nguvu yetu walitufanyia hujuma kwa wagombea wetu,” anasema.

Mnyika anatumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutumia kila mbinu kudai tume huru ya uchaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu mwaka huu.

“Tunaomba wananchi waliopo vijijini, wanaotumia mitandao ya kijamii na kila mmoja atumie kila njia kudai tume huru ya uchaguzi,” anasema Mnyika.

Anasema ingawa Rais ametangaza uchaguzi huo utakuwa huru, kauli hiyo haipaswi kuaminiwa kwa kuwa tume iliyoharibu uchaguzi wa Serikali za mitaa bado ipo pamoja na wakurugenzi na watendaji wengine wa Serikali ambao wanasimamia uchuguzi.

“Watanzania tusimame kumtaka Rais apeleke bungeni muswada kwa hati ya dharura katika Bunge linaloanza kesho (leo) ili yafayike mabadiliko na ipatikane tume huru ya uchaguzi,” anasema.

Anaeleza kuwa pamoja na hayo wataendelea kutumia mitandao ya kijamii kujiimaisha ingawa nguvu kubwa bado ipo, ni msingi.

ACT Wazalendo

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu anasema CCM ina hofu ya kushindwa na vyama vya upinzani kwa kuwa haijafanya mambo ya kutosha kuwaridhisha wananchi.

“Katika kipindi cha miaka minne CCM imefanya miradi mingi ambayo bado ipo katika hatua za awali. Mfano reli, umeme na ujenzi wa miundombinu, huku hali ya maisha ya wananchi ikiwa bado haijatengemaa,” anasema.

Ado anasema hali hiyo inachangia CCM kutojiamini mbele ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu. “CCM ni dhaifu na kinaweza kushindika na vyama vya upinzani,” anasema.

NCCR Mageuzi

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza anasema hofu ya CCM inatokana na kujiendesha kama chama dola badala ya chama cha siasa.

Anasema hali hiyo inatokana na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi za chini kutozuiwa kufanya mikutano ya kisiasa eneo lolote.

“Viongozi wa CCM wakitaka kufanya mikutano sehemu yoyote wanaruhusiwa hata wakiwa viongozi wa kijjiji au kata, lakini kwa upinzani wanazuiwa kwa madai ya intelejensia kutoruhusu,” anasema.

Anasema kuwa hali hiyo inashangaza na kutoa mfano baba kuendelea kumlea mtoto mwenye umri wa miaka 40, huku akimtaka wa miaka 20 akajitegemee na kuelezea hata majirani watahoji kuwa jambo halijakaa sawa.

Ruhuza anasema kutokana na hali hiyo wananchi wanapata ujumbe kwamba wapinzani wana hoja za kuzungumza, lakini wanazuiwa ili wasizifahamu.

“CCM pamoja na kuwa huru kufanya siasa, imekuwa haipati uungwaji mkono kutoka kwa wananchi kwa kuwa wanashindwa kubadilika katika mbinu za ufanyaji siasa. Anayeweza kubadili hali hiyo ni mwenyekiti wa chama,” anasema na kuongeza:

“Kinana na Nape walipokuwa viongozi ndani ya CCM walisaidia kukijenga chama na kukirudisha kwa wananchi kwa sababu walikuwa wakiruhusu ukosoaji, hivyo walikuwa wakiongea lugha moja na wananchi.”

Anasema hali ya sasa ni tofauti na viongozi wanaokosa ndani ya chama hicho wanaonekana maadui, hali ambayo inazua maswali kwa wananchi.

“Wananchi sasa wanapima na kuona wapinzani wana hoja nzito ambazo watawala hawataki zifahamike kwa wananchi. Hali hiyo imesababisha chama hicho kupoteza umaarufu. Kwa kifupi CCM inajimaliza yenyewe,” anasema.

Anatoa mfano wa hivi karibuni ambako mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alizuiwa kufanya mikutano, lakini Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliruhusiwa.