Wasaidizi 100 wa kisheria Zanzibar wafundwa

Muktasari:

Kesi zinazotatuliwa kwa wingi na paralegal ni pamoja na kesi za ardhi, ndoa, matunzo kwa watoto, jinai, na ukatili wa kijinsia.

Dar es Salaam. Zaidi ya wasaidizi 100 wa kisheria visiwani Zanzibar wamepewa mafunzo kuhusu sheria zilizopo, kanuni, miongozo na sera zinazohusiana na kazi yao ya kisheria.
Wasaidia hao wa msaada maarufu kama paralegal wamepewa mafunzo  na mbinu ziakazowawezesha kuendelea kutoa elimu na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi bila malipo yoyote na kuwezesha upatikanaji wa haki hasa kwa wanawake
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rashid Hassan Mshamata kutoka Wete alisema mafunzo hayo yamewasaidia na kuwapa mbinu mpya za kutumia wakati wa kutoa msaada wa kisheria pamoja na elimu kwa jamii.
Alisema wakati wa mafunzo wametakiwa kutumia uwezo na ujuzi kwenye kazi zao za kila siku wakifuata taratibu na kanuni zilizopo pamoja na kuongeza ushirikiano.
Zaina Omari Othman wa Micheweni alisema mafunzo hayo yamekuwa zana muhimu ya uwezeshaji kwao katika kutekeleza majukumu yao juu ya msaada wa kisheria kwa jamii
"Tunafurahi kujifunza vitu vipya ambavyo vimeongeza thamani katika uelewa wetu juu ya maswala kadhaa ya kisheria ambayo yataleta tija katika jamii tunayoitumikia na kutuwezesha kufanya kutoa msaada wa kisheria kwa watu walio na mahitaji maalumu katika jamii," alisema   
Afisa Programu ya Uwezeshaji kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Legal Services Facility (LSF) Victoria Mshana alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi wasaidizi wa kisheria pamoja na kujua mabadiliko mapya ya kisheria kwa Zanzibar.
Alisema Shirika hilo limewawezesha paralegal zaidi ya 3950 walioko kila wilaya Tanzania bara na Zanzibar kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii bure bila malipo yoyote.
 “Kwa wastani kwa mwaka paralegal usaidia takribani kesi 70,000 ambazo asilimia 60 ya kesi hizi wanazitatua wakati asilimia 22 zinakuwa bado zinaendelea asilimia 16 zimepelekwa kwa vyombo vya juu kwa utatuzi huku asilimia 2 ya kesi zinazowafikia zikishindwa kupatikana usuluhishi. 
Alifafanua kwamba kesi zinazotatuliwa kwa wingi na paralegal ni pamoja na kesi za ardhi, ndoa, matunzo kwa watoto, jinai, na ukatili wa kijinsia.