Wasambaza taarifa za uongo kuhusu madhara ya dawa kushughulikiwa

naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile

Muktasari:

Serikali ya Tanzania ipo mbioni kuanza kuwachukulia hatua wanaosambaza katika mitandao ya kijamii  taarifa za uongo kuhusu madhara anayoweza kuyapata mtu iwapo atatumia aina fulani ya dawa.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania ipo mbioni kuanza kuwachukulia hatua wanaosambaza katika mitandao ya kijamii  taarifa za uongo kuhusu madhara anayoweza kuyapata mtu iwapo atatumia aina fulani ya dawa.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Agosti 29, 2019 na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) akiongozana na kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Amesema dawa zinazouzwa nchini huthibitishwa ubora wake na TMDA kabla ya kuuzwa na hakuna dawa iliyo bora zaidi ya nyingine.

“Niwaombe wananchi kutosambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo, kama wana swali au hoja kuhusu ubora wa dawa ni bora wawasiliane na TMDA kwa sababu sasa tutaanza kuchukua hatua kwa upotoshaji usio na msingi,” amesema Dk Ndugulile.

Amesema wananchi hawapaswi kuwa na mashaka na dawa zinazouzwa katika maduka kwa sababu maabara ya TMDA inaongoza kwa ubora barani Afrika na wapo katika mkakati wa kuomba kibali cha kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Tukipata kibali majibu ya vipimo tutakayokuwa tunayatoa Tanzania yatakuwa yanakubalika dunia nzima na itakuwa ni hatua kubwa kwetu,” amesema Dk Ndugulile.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Mohammed Dimwa amesema ubora wa maabara ya TMDA na viwango vyake umewapa  nguvu ya kuishawishi Zanzibar kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kununua mashine za kupima dawa zao wenyewe.