Wasira amjibu Zitto kuhusu wanaopata mimba kuendelea na masomo

Muktasari:

Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Stephen Wasira amemjibu kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyeiandikia barua Benki ya Dunia (WB) kuishawishi kutoipatia Tanzania fedha kwa ajili ya sekta ya elimu.

Dar es Salaam. Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Stephen Wasira amemjibu kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyeiandikia barua Benki ya Dunia (WB) kuishawishi kutoipatia Tanzania fedha kwa ajili ya sekta ya elimu.

Moja kati ya hoja za Zitto katika barua hiyo ni kwamba fedha hizo hazitatumika kama ilivyoelezwa kwa kuwa nchini Tanzania watoto wanaopata mimba wakiwa shule hawapewi nafasi ya kurudi shule kuendelea na masomo.

Akihojiwa leo Jumatatu Februari 10, 2020 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds,  Wasira amesema Zitto si mzalendo kunapokuwa na jambo lenye maslahi ya Taifa nchi kubwa kama Marekani huwa wanaweka tofauti zao pembeni na wanaungana.

Wasira amesema alimsikiliza Zitto walipohojiwa mjini Washington DC, Marekani na  aliwasikiliza na Watanzania wanasemaje kuhusu hoja hiyo.

Yupo Mtanzania mmoja anaitwa Salma alimuuliza Zitto swali hili, “lakini wewe (Zitto) sasa unataka benki isitoe mkopo, kwa kufanya hivi si unawaumiza Watanzania wengi zaidi kuliko kuwasaidia, inasaidia nini?”

Wasira amesema katika majibu yake Zitto amesema, “ilani (ya CCM)  ilisema wakipata mimba wasome.”

Waziri huyo wa zamani akieleza mtazamo wake kuhusu majibu na hoja ya Zitto amesema, “mimi ningekuwa kijana kama Zitto ningemjibu na hata kama mimi sio kijana ninaweza kumjibu kwa sababu hoja zake zinajibika.”

 “Msingi wetu ni kusomesha watoto, kupata mimba ni changamoto inayotokana na gender (jinsia), nafikiri watu wazima ambao lengo letu ni kuwasomesha watoto wote lakini ipo changamoto, kuzuia pesa kutoka benki ya dunia sio jibu.”

“Mimi ningefikiri vijana wote wangekaa chini pamoja na Zitto tuseme benki lazima itupe pesa lakini tutazame ili tusaidie wasichana wanaopata mimba tunawasaidiaje, kuwaambia tu mtarudi shule sio jibu peke yake, ila inatakiwa kuwasaidia kutopata mimba kwa hiyo benki itupe pesa ili tuwajengee hosteli, maeneo ambako tumejenga hosteli mimba zimepungua,” amesema Wasira.

Ameongeza, “Si wanataka kuwatengenezea watoto wa sekondari, kwa hiyo watupe pesa ili tuwajengee hosteli. Sisi kama chama kikubwa cha siasa hatuwezi kuwaambia watoto zaeni tu, kujenga nchi ni pamoja na kujenga tabia.”

Huku akiwa makini Wasira amesema, “tunatakiwa kuwaambia wasichana someni na kuwajengea mazingira yanayowapa unafuu, mfano usafiri msichana anapotembea kwa miguu hata lifti ya baiskeli inaweza kuwa kishawishi cha kupata mimba.”

“Hoja hapa ni kuweka miundombinu mizuri ili wasipate mimba, lakini anachozungumza Zitto ni kama kuwaambia zaeni tu.”

Kuhusu wanaume wanawapa mimba wanafunzi, Wasira amesema sheria ipo, “na inawahusu watia mimba, tena wanaotia mimba ndio wanaoshughulikiwa na sheria, ipo tena wanasema kwa nini inawaadhibu wanaume tu wakati hao walikubaliana.”