Wasomi UDSM waeleza watakavyoazimisha Desemba 9

Friday December 6 2019

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jumuia wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa) nchini Tanzania imeandaa mdahalo wa kujadili na kutafakari kuhusu nafasi, wajibu na mchango wa wanataaluma katika maendeleo ya taifa.

Mada kuu ya mdahalo huo utakaofanyika Desemba 9, 2019  ni ‘Miaka 58 ya Uhuru: Wajibu na Mchango wa Wanataaluma Katika Maendeleo ya Taifa’.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Desemba 6, 2019 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Udasa, Dk George Kahangwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Dk Kahangwa amesema mdahalo huo utatoa nafasi kwa wanataaluma na wadau wengine wa maendeleo katika umma wa Tanzania pamoja kujadili na kutafakari kuhusu nafasi, wajibu na mchango wa wanataaluma katika maendeleo ya Taifa.

“Mdahalo huo utafanyika hapa Chuo kikuu Mlimani kwenye ukumbi wa Nkrumah saa 8:00 mchana.”

“Huu ni mdahalo wa aina yake na wa kipekee kwani tangia nchi ipate uhuru hatujawahi kupata nafasi ya kutosha, umma Watanzania ukapata fursa huru na ya wazi ya kutathmini mchango na wajibu wa wanataaluma na wasomi wengine kwa ujumla katika maendeleo ya taifa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa,” amesema Dk Kahangwa.

Advertisement

Amesema wametayarisha mdahalo huo kwa sababu wanaamini safari iliyo mbele kama taifa inahitaji mshikamano na ushirikiano wa karibu kati ya wasomi na makundi yote ya kijamii kutatua changamoto za taifa  na kuleta maendeleo ya Watanzania wote katika uhalisia wa maisha yao.

“Udasa tumeandaa mdahalo huu kwa nia ya dhati tukiamini usomi wetu hauwezi kuwa na maana kwa Watanzania kama hatuelewi wanategemea tuwe tukiwafaa kwa njia zipi.

“Huenda tunafahamu wajibu wetu kama wanataaluma, lakini si vyema tukibakia kudhani kuwa ndio wajibu wetu na huku Watanzania wanategemea vinginevyo kinyume na tunavyofanya,” amesema Dk Kahangwa

Alisema watakuwa na  muda wa kutosha kuruhusu kila aliye kuja na nia ya kuchangia hoja kufanya hivyo. 

Alifafanua kutakuwa na wazungumzaji wakuu, lakini kazi yao itakuwa ni kutoa mwanga kuhusu wajibu na mchango uliotolewa na wanataaluma katika kuijenga Tanzania katika zama tofauti.

“Hii itatusaidia kujiona wapi tunahitaji kujifunza ili kuifanya taaluma yetu iwafae Watanzania,” amesema

Advertisement