VIDEO: Watakaobainika kuihujumu Serikali ya Tanzania kushtakiwa

Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas

Muktasari:

  • Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema mtu yeyote atakayebainika kuihujumu Serikali atafunguliwa mashtaka.

Dodoma. Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema Serikali haitarudi nyuma katika kusukuma mbele maendeleo ya Watanzania na kama kuna mtu anaihujumu nchi katika masuala yoyote, ajue sheria za nchi zipo.

Amesema akichukuliwa hatua, asije akalalamika kuwa haki zake za binadamu  zinavunjwa.

Dk Abbas ameyasema hayo Jijini Dodoma leo Jumamosi Agosti 31, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema wapo Watanzania wanashiriki kuihujumu Serikali  lakini wakumbuke kuna siku uhujumu huo hautawasaidia.

“Wapo wazawa wanaofanya mawili matatu kuhujumu nchi lakini niwaeleze hakuna Nabii katika historia ya Manabii aliyewahi kuaminiwa kwa asilimia 100, hivyo huwezi kukubaliwa na watu wote, hata hii ndege inayoshikiliwa ikija Tanzania ipo siku wanaochukia watatumia usafiri huo kwenda Afrika Kusini kama sio wao basi watoto wao,” amesema Dk Abbas.

 

Amesema Serikali, wameamua kuibadilisha nchi na katu hawatarudi nyuma, bali wanafanya yale ambayo wanaamini kuwa yatabadilisha nchi.

“Ujumbe kwa hawa wanaofanya mawili matatu, nchi hii ina sheria na si kazi yangu kutaja majina ya watu, hata katika historia ya manabii, aliyewahi kukubalika kwa asilimia 100.”

“Hivyo hata sisi wa Serikali ya Awamu ya Tano tunafanya yale ambayo mioyoni mwetu tunaamini kuwa yataiokoa na kuibadilisha hii nchi,” amesema msemaji huyo mkuu wa Serikali.

 Amesema wanaopinga na kubeza kifanywacho na Serikali ipo siku moja kitawasaidia.

Ametolea mfano wa Mradi wa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa maji katika Mto Rufiji kuwa ni wa Watanzania wote na kila mmoja utamsaidia.

Pia,  amesema hata wanaofurahi kukamatwa kwa Ndege ya Tanzania nchini Afrika Kusini ipo siku watakuja kuitumia kusafiria.

“Yeyote anayehujumu chochote, afahamu kwamba iko siku itamsaidia yeye na familia yake au kizazi chake cha baadaye,” amesema.

Ametolea mfano, kuwa kama mtu akiihujumu ndege ambayo ni ajira na ni mapato kwa Serikali, “Kwa hiyo ukiihujumu ndege hujamuhujumu Dk Abbas au Rais Magufuli (John) bali unakuwa umehujumu mapato ya nchi na umehujumu vizazi vijavyo,” amesema Dk Abbas.