VIDEO: Watalii 64 watembelea Tanzania kwa kutumia treni ya Tazara

Saturday October 12 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watalii 64 wamewasili leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 nchini Tanzania kwa kutumia Reli ya Tazara kwa lengo la kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Watalii hao wametokea Afrika Kusini wakitumia treni ya kifahari ya kampuni ya Rovos Rail ya nchini humo wakitumia siku 15.

Wakiwa na bashasha na hamasa kubwa watalii hao walishuka kwenye treni na kuanza kusakata muziki uliokuwa ukipigwa na bendi ya polisi.

Watalii hao walieleza kuvutiwa na hali ya hewa ya Tanzania na shauku kubwa ya kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga ya Serengeti, mapambo ya Bagamoyo na Zanzibar.

“Nimevutiwa na hali ya hewa na ukarimu wa Watanzania natamani zaidi kufika Zanzibar nimekuwa nikisoma na kuangalia picha za visiwa hivyo kwa muda mrefu,” amesema John Macmillian.

Ofisa uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),  Agustina Makoye amesema ujio wa treni hiyo una tija kubwa kwa sekta ya utalii nchini.

Advertisement

“Ugeni huu ni mkubwa na una faida kwa Taifa kwanza ni treni ya kifahari, inawaleta watu kutoka mataifa mbalimbali hoteli zitafanya biashara na hata vivutio vya utalii vitaingiza fedha kupitia watalii hawa hivyo tunaamini kuwa Rovos ina mchango mkubwa kwa utalii wa Tanzania,” amesema Makoye.

Advertisement