Watano mbaroni polisi wakipambana na madereva Bajaj Iringa

Tuesday October 22 2019

Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa Juma Bwire

Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa Juma Bwire akizungumza na wanahabari kuhusu tukio la askari polisi kutawanya wananchi kwa kupiga mabomu 

By Berdina Majinge, Mwananchi [email protected]

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linawashikilia watu watano baada ya kuibuka vurugu kati yake na madereva Bajaj  katika mtaa wa Frelimo mkoani humo.

Katika vurugu hizo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya madereva hao waliopinga kitendo cha mwenzao kukamatwa.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 22, 2019 kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema tukio hilo limetokea leo saa 5 asubuhi baada ya polisi  kumkamata dereva Bajaj aliyekuwa amepakia abiria sita kinyume na taratibu.

Amesema polisi wakiwa katika operesheni ya kukusanya madeni walipoiona Bajaj hiyo waliikamata kwa lengo la kuipeleka kituo cha polisi.

“Askari mmoja aliingia katika Bajaj kwa lengo la kuipeleka kituoni lakini wakiwa njiani dereva aliipindua akiwa na lengo la kuipeleka kwenye kijiwe chao kumzuia askari kutekeleza majukumu yake.”

“Dereva wa Bajaj alikuwa akisema ‘leo nitakufanyia kitu mmezoea kutukamata kila siku’. Baada ya Bajaj kupinduka madereva wengine walianza kumshambulia askari ambaye aliomba msaada kwa wenzake waliokuwa doria ambao walifika kutafuta mwafaka lakini walirushiwa mawe,” amesema kamanda huyo.

Advertisement

Amesema katika vurugu hizo kioo cha gari la polisi kilivunjwa, kusisitiza kuwa Bajaj tano na pikipiki moja zinashikiliwa na polisi.

Mmoja wa mashuhuda kwa sharti la kutotajwa jina amelieleza Mwananchi kuwa alipokuwa mtaa wa Frelimo alishuhudia Bajaj ikiyumba na kupinduka, “niliwaona dereva na askari wakitoka katika Bajaj hiyo. Nilishangaa kuona askari wakimpiga dereva ndipo tulisogea kuona nini kinaendelea, tukaamua kumsaidia mwenzetu.”

Advertisement