Watano wauawa kwa risasi Marekani

Muktasari:

Mamia ya watu wamekuwa wakiuawa kila mwaka nchini Marekani kwa kupigwa risasi, jambo ambalo liliwasukuma wanaharakati nchini humo kushinikiza kufanyia marekebisho sheria za umiliki wa silaha ili kudhibiti mauaji hayo.

Texas, Marekani. Watu watano wameuawa na wengine kujeruhiwa baada ya mtu mwenye silaha kuliteka nyara gari la huduma za posta huko Texas Magharibi nchini Marekani na kuwamiminia watu risasi.

Tukio hilo lilitokea jana Jumamosi ya Agosti 31,2019 usiku ambapo mtu huyo ambaye bado hajatambuliwa kwa jina alitekeleza mauaji hayo. Polisi wanasema mtu huyo ni kijana wa miaka 30.

Mtu huyo aliwafyatulia risasi watu zaidi ya 20, hata hivyo, polisi bado haijathibitisha iwapo mtu huyo aliuwawa au ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika mkasa huo uliotokea maeneo ya Odessa na Midland.

Shirika la Habari la DW lilimnukuu mkuu wa polisi wa Odessa, Michael Gerke akisema mbali na maofisa wa polisi waliojeruhiwa wapo raia 21 ambao wameathiriwa na tukio hilo.

Ripoti ya awali ya polisi inaonesha kulikuwa na zaidi ya mtu mmoja aliyekuwa akifanya mashambulizi ingawa mamlaka katika eneo la tukio imesema kulikuwa na mshambuliaji mmoja tu.

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence alisema utawala wa Rais Donald Trump unadhamiria kufanya kazi na vyama vyote kukabiliana na matukio ya udhalimu dhidi ya raia wa Marekani. 

Marekani imekuwa ikikabiliwa na visa vya mauaji ya watu kwa kupigwa riasasi huku kukiwa na mvutano kuhusu sheria za umiliki wa sialaha nchini humo.

Mamia ya watu wamekuwa wakiuawa kila mwaka nchini humo kwa kupigwa risasi, jambo ambalo liliwasukuma wanaharakati nchini humo kufanyia marekebisho sheria za umiliki wa silaha ili kudhibiti mauaji hayo.

Mwaka 2013 pekee, watu 33,636 waliuawa kwa risasi nchini humo wakati wengine 73,505 wakijeruhiwa. Takwimu hizo zinahusisha matukio ya kuua watu, kujiua au kujipiga risasi kwa bahati mbali.