Watatu kizimbani kwa kuchoma moto ofisi ya kanisa

Muktasari:

Watu watatu wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kuchoma moto ofisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Misungwi na kusababisha hasara ya mali na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh12.3 milioni.

Misungwi. Watu watatu wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kuchoma moto ofisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Misungwi na kusababisha hasara ya mali na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh12.3 milioni.

Waliofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu mkazi Wilaya ya Misungwi, Erick Marley ni pamoja na Emanuel  Marco (25), Edison  Jonathan (23) na Ally Juma (23) ambaye ni mlinzi wa kanisa hilo ambao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo usiku wa kuamkia Machi 15, 2020.

Akisoma hati ya mashtaka katika kesi hiyo ya jinai namba 39/2020, mwendesha mashitaka wa Polisi, Ramsoney Salehe aliiambia Mahakama kuwa kosa hilo lilitendeka eneo la kijiji cha Misungwi kinyume cha kifungu 319 (a) (e) cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2002.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na kuachiwa kwa dhamana ya Sh15 milioni kila mmoja. Shauri hilo litatajwa tena Aprili Mosi, 2020.