Watatu wauawa, mwenyekiti wa mtaa akamatwa Mwanza

Muktasari:

  • Watu watatu wamefariki dunia baada ya kufungwa kamba na kupigwa kwa mawe na wana mtaa wakiwatuhumu kuwa wezi na wabakaji. Katika tukio hilo watu watano wamekamatwa akiwemo mwenyekiti wa mtaa.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza nchini Tanzania linawashikilia watu watano akiwamo mwenyekiti wa mtaa wa Nyakabungo A wilayani Nyamagana, Abdulkadiri Yunusu wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya watu watatu wakiwatuhumu kujihusisha na vitendo vya wizi na ubakaji mtaani hapo.

Taarifa ya Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro aliyoitoa kwa vyombo vya habri leo Jumatatu Desemba 2, 2019 imesema tukio hilo lilitokea Desemba Mosi, 2019 saa 1:45 jioni.

Kamanda Muliro amewataja waliouawa ni Dotto Constantine (19), Bakari na mwingine hakufahamika jina, wote wakazi wa Nyakabungo wilayani Nyamagana.

Pia, amewataja waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo mbali na mwenyekiti ni; Chacha, Ramadhan Athman na Hamis Peter wote wakidaiwa kuhusika kuwafunga Kamba.

“Vijana hao (marehemu) walikuwa wakipita ndipo walikutana na watu walioanza kuwakimbiza na baadaye mwenyekiti mtaa huo aitwaye Abdulkadiri Yunusu alipiga firimbi huku akitamka kuwa watu hao ni wezi ndipo walikamatwa na kufungwa kamba kisha kuwapiga mawe hadi kufariki dunia,” amesema Muliro

Amesema bado upelelezi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani, huku wakiendelea kuwafuatilia watu wengine walioshiriki kwa namna moja ama nyingine katika tukio hilo.