Watendaji wa vijiji wafunga ofisi, wagombea washindwa kurejesha fomu

Monday November 4 2019

By Waandishi wetu , Mwananchi [email protected]

Arusha. Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha kimelalamikia wagombea wake katika uchaguzi mdogo wa serikali za mtaa  zaidi ya 100 kushindwa kurejesha fomu baada ya watendaji wa vijiji na Kata kufunga ofisi tangu asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 4, 2019, Katibu wa Chadema Mkoani Arusha, Elisa Mungure amesema jitihada za kuwatafuta viongozi hao tangu asubuhi zimekwama katika vijiji vingi vya wilaya za Arusha, Arumeru, Monduli, Longido na Karatu.

"Tumeandika malalamiko yetu kwa wasimamizi wa uchaguzi lakini hatujui hatma yake, hivyo tunaomba wanahabari mtusaidie kufikisha hizi taarifa ili watu wajue rafu tunazochezewa,” amesema Mungure.

Amesema licha ya watendaji kufunga ofisi, baadhi ya wagombea wameporwa fomu zao, wengine wamekamatwa na kundi la  vijana.

“Huu si uchaguzi, ni vurugu wenzetu CCM wagombea wao wamejaza fomu na kupelekwa majumbani kwa watendaji wa vijiji na Kata ili kuhakikisha wagombea wa upinzani hawarudishi fomu,” amedai Mungure.

Katibu wa Chadema wilayani Arusha, Innocent  Kisanyage  amedai kuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti katika  Mtaa wa Masikiria Kata ya Terrati, Justine Laizer alivamiwa juzi usiku na na watu waliodaiwa kuwa ni polisi.

Advertisement

Amedai wasimamizi wa uchaguzi wasaidizi  Kata ya Sombetini Mtaa wa  Simanjiro na Olmuriaki nao wamegoma kupokea fomu za wagombea wa Chadema na tayari chama hicho kimeandika barua za malalamiko.

“Tumeandika barua kwa msimamizi wa uchaguzi juu ya matukio haya na ukiukwaji kwa kanuni na kumpa nakala waziri mwenye dhamana,” amesema.

Kisanyage alitaja mitaa mingine  ya Jiji la Arusha ambayo wagombea wake wamekumbwa na kadhia hiyo ni mtaa wa Sokoni One, Muriet, Olmoriaki  na Longdong.

Baadhi ya wagombea hao waliokumbwa na kadhia hiyo, Clotilda Aloyce anayegombea Mtaa wa  Olmuriaki, Kata ya Sombetini amedai wakiwa katika ofisi ya Ofisa Mtendaji, walivamiwa na watu wasiojulika wakawa wanawashambulia kwa kipigo na kuwataka wawapatie fomu

Renatus Kimario mgombea wa Mtaa wa Kijenge Kaskazini, Kata ya Kimandolu amedai kuwa juzi wakiwa wanahakiki fomu majira ya saa saba mchana, walivamiwa  na watu watatu wakiwa na gari nyeupe  waliwatishia kwa silaha na kuzichukua fomu zao na kuondoka kwa kasi .

Akizungumzia kadhia hizo, Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Arusha Mjini, Msena Binna amekiri kupokea malalamiko juu ya watendaji kutoonekana kwenye ofisi zao na kudai kuwa suala hilo wamelishughulikia kikamilifu.

“Kwa upande wangu sina taarifa za mgombea kutekwa ila kama kuna mtu ametekwa anapaswa kutoa malalamiko polisi kwa sababu ni kosa la jinai,” amesema.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana akizungumza na Mwananchi juu ya saga hilo amesema matukio hayo yanachunguzwa na ikibainika kuna watu wamekiuka sheria, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao .

“Kuna kanuni na taratibu za uchaguzi zinapaswa kufuatwa pale ambapo mgombea anaona ananyimwa haki yake,” amesema Kamanda Shana.

Advertisement