Watoto 21 kati ya 1000 wanafariki kwa kuzaliwa kabla ya wakati

Friday November 22 2019

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watoto wachanga 21 katika vizazi hai 1000 wanakufa kwa sababu ya kuzaliwa kabla ya wakati.

Takribani watoto milioni 1.5 wanazaliwa nchini Tanzania, kati yao asilimia 10 sawa na watoto 255,000 wanazaliwa wakiwa njiti.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 22, 2019  jijini Dar es Salaam na daktari bingwa wa watoto wa Hospitali ya Aga Khan, Yaser Abdallah wakati wa maadhimisho ya siku ya watoto njiti katika hospitali hiyo.

Dk Abdallah amesema mambo yanayochangia mtoto kuzaliwa kabla ya wakati ni pamoja na maradhi ya mama, udhaifu wa mlango wa kizazi, kuwa na mapacha au historia ya kuwahi kujifungua njiti siku za nyuma.

"Tunashauri mama akigundua ana ujauzito aaanze kuzingatia ratiba ya kliniki sambamba na kufanya vipimo vya mara kwa mara," amesema daktari huyo.

Dk Abdallah amesema watoto wanaozaliwa njiti wana uwezekano mkubwa wa kupata ulemavu, na kwamba inatumia nguvu kubwa kuwasaidia watoto wanaozaliwa chini ya wiki 30 za ujauzito.

Advertisement

Mkuu wa Idara ya Watoto wa hospitali hiyo, Dk Mariam Noran amesema wanatoa huduma kwa watoto wanaozaliwa na uzito pungufu kuanzia gramu 700 na kuwawezesha kuishi.

Amesema katika hospitali hiyo, wanazaliwa watoto 100 - 150 kwa mwezi. Dk Noran amesema wanalaza watoto 30 kati yao 15 wanakuwa wamezaliwa njiti.

Akitoa uzoefu wake, mama aliyejifungua mapacha wanne njiti mwaka 2017, Beatrice Malawa amesema wanaojifungua watoto njiti wanaathirika kisaikolojia ameshauri wanawake kupewa ushauri na kukabiliana na hali iliyojitokeza.

Advertisement