Watoto 6,927 nchini Tanzania watoa taarifa ukatili wa kijinsia

Thursday February 13 2020

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watoto 6,927 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia walitoa taarifa ya vitendo walivyofanyiwa kwa kutumia simu baada ya kupiga namba 116 ambayo ni bure, kati ya mwaka 2013/2014 hadi 2018/2019.

Mbali na watoto hao pia watu 116,889 waliripoti matukio ya ukatili wa kijinsia waliyofanyiwa kupitia madawati maalumu 420 yaliyopo sehemu mbalimbali nchini Tanzania kati ya mwaka 2016 hadi 2018.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 13, 2020 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika mkutano na waasisi wa umoja wa jumuiya ya wanawake katika nchi huru za Afrika (Pawo) tawi la Tanzania.

Mkutano huo ulilenga kupitia na kupokea maoni kwenye rasimu ya sera ya  wanawake na jinsia ambayo inafanyiwa mapitio.

Akizungumza katika mkutano huo, Ummy amesema kuanzishwa kwa simu ya bure kwa ajili ya kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kumechangia kuongeza kasi ya upataji wa taarifa kwa haraka.

“Watoto ambao hufanyiwa vitendo hivi huunganishwa na huduma mbalimbali za kijamii kama polisi, ustawi wa jamii na Mahakama,” amesema Ummy.

Advertisement

Ummy ametumia nafasi hiyo pia kuonyesha masikitiko yake namna gani kukosekana kwa ukaribu kati ya watoto na wazazi kunavyowafanya  watoto kufanyiwa ulawiti huku wazazi wakishtuka wakati hali imeshakuwa mbaya.

Alisema inashangaza kuona mtoto anayeishi na wazazi wake kufanyiwa vitendo vya ulawiti hadi kwa miezi mitatu mfululizo bila wao kujua.

“Hivi inakuwaje mtoto analawitiwa mwezi wa kwanza, pili, tatu na baba yupo na mama yupo tunakosea wapi? Ina maana mkirudi nyumbani hamzungumzi na watoto wenu, mnaendeleaje mmeshindaje.”

“Yaani wakati mwingine unapokea kesi unaona kabisa mzazi amegundua mwanae akifanyiwa vitendo hivyo na ameshaharibiwa, ndiyo maana juzi bungeni kulikuwa na mjadala kuwa wanaume wanaolawiti wahasiwe lakini tuliona haitatusaidia kwa sababu hata miaka 30 ni mingi lakini watu hawaogopi,” amesema Ummy

Ameitaka jamii na wazazi kusimama pamoja  kuhakikisha wanapigania haki za watoto na kuondoa vitendo hivyo.

Makamu Mwenyekiti wa Pawo, Lea Lupembe amesema wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kuongeza msukumo wa kuwashirikisha wanawake wa barani Afrika katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Yote haya yamekuwa yakifanyika ili kuhakikisha tunajenga usawa wa kijinsia kwa wanawake na hata jamii kwa ujumla,” amesema Lea.

 

Advertisement