Watoto watatu wa familia moja wafariki katika ajali ya moto

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Ukerewe Eren Rock (kushoto) akimpa pole mama wa watoto watatu waliopoteza maisha kwa moto kisiwani Ukara jana. Picha Jovither kaijage

Muktasari:

Watoto watatu wa familia moja wakazi wa kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wamefariki baada ya chumba walichokuwa kuungua kwa moto.

Ukerewe. Watoto watatu wa familia moja wakazi wa kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wamefariki baada ya chumba walichokuwa kuungua kwa moto.

Watoto hao ni ni Rea Crizant (5), John Kamugisha(3) na Veronica Baraka (2).

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 24, 2019 na katibu tawala wa wilaya ya Ukerewe, Focas Majumbi inaeleza kuwa tukio hilo limetokea jana Ijumaa saa 10 jioni katika kitongoji cha Ebugwe.

Mganga mkuu wa kituo cha afya Bwisya, Dk Joakimu Kole amesema watoto hao walifikishwa katika kituo hicho saa 11 jioni  lakini kutokana na kuungua kwa kati ya asilimia 65 hadi 100, wote walifariki dunia.

Amesema jitihada za kuwapatia matibabu zilifanyika kwa kiwango kikubwa lakini ilishindikana.

Mkuu wa kituo cha polisi Ukara, Joseph Paul akithibitisha tukio hilo, amesema uchunguzi wa awali unaonyesha moto huo ulitokea  baada ya mmoja wa  watoto hao kuwasha moto kwa kutumia kiberiti na ukashika nguo, godoro na chandarua.