VIDEO: Watu sita wauawa wilayani Tandahimba

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai DCI Robert Boaz (aliyevaa kiraia) na Kamishna wa operesheni na mafunzo CP Leberatus sabas wakizungumza na wakazi wa kijiji cha Misufini kilichopakana na kijiji cha Ngongo  wilaya ya Tandhimba mkoa wa Mtwara baada ya kutokea mauaji ya watu sita na wengine watano kujeruhiwa.Picha na Mpiga picha wetu

Muktasari:

Watu sita wameuawa katika kijiji cha Ngongo Wilaya ya Tandahimba mkoani  Mtwara na wengine saba kujeruhiwa katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Jumanne Novemba 12, 2019.

Mtwara. Watu sita wameuawa katika kijiji cha Ngongo Wilaya ya Tandahimba mkoani  Mtwara na wengine saba kujeruhiwa katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Jumanne Novemba 12, 2019.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema Watanzania sita walipigwa risasi na watu wanaodhaniwa kutoka nchi jirani ya Msumbiji wakati wakiwa visiwa vya mto Ruvuma wanakofanya shughuli za kilimo.

“Usiku walivamiwa na kikundi cha watu waliowakusanya pamoja na kuwapiga risasi. Watu sita walifariki dunia na wengine saba walijeruhiwa na wamelazwa Hospitali ya Tandahimba.”

“Jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola tutachukua hatua madhubuti kuhakikisha wote waliohusika na tukio hili wanapatikana na kuchukuliwa hatua,” amesema DCI Boaz.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na kuwataka wananchi kuchukua tahadhali wanapokwenda nchi nyingine kufanya shughuli za kiuchumi.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Liberatus Sabas amesema kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ndio maana wahalifu wanafanya matukio hayo mipakani.

“Tusikubali hata siku moja wavuke mpaka waje huku ndani tupo bega kwa mbega na wananchi. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo pamoja tutawasaka, tutawatia mbaroni na hatua kali zitachukuliwa.”

“Kama alivyosema (Boaz) wengine wako humuhumu ndani tuwafichue pamoja, sisi tunaelekea eneo la tukio lakini tone la damu ya Mtanzania haliwezi kupotea bure,” amesema.