Watu tisa wafariki dunia katika maandamano Guinea

Muktasari:

Ni baada ya polisi kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji wanaopinga mabadiliko ya Katiba yanayompa Rais wa sasa kuwania kipindi cha tatu.

Guinea. Jeshi la Polisi la Guinea imethibitisha watu tisa wameuawa katika maandamano ya wananchi yanayoendelea nchini humo.

Wananchi nchini Guinea kwa zaidi ya wiki moja sasa wanaandamana wakipinga mabadiliko ya Katiba yanayopangwa kufanywa na utawala ili kuruhusu Rais Alpha Conde kugombea kipindi cha tatu.

Rais Conde ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 81 aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2010. Mwaka 2015 alichaguliwa tena ambako kipindi chake cha pili kinatarajiwa kuisha 2020.

Hata hivyo, kabla ya kumaliza kipindi chake kiongozi huyo tayari ameshaonyesha nia ya kutaka kuwania awamu nyingine ya kipindi cha tatu na kutaka Katiba kufanyika kwa mabadiliko ili kumuwezesha kuwania nafasi hiyo.

Mmoja wa mashuhuda walioshuhudia tukio hilo alililiambia Shirika la habari la Reuters kuwa polisi waliwafyatulia risasi za moto waandamanaji waliokuwa wamefunga barabara kwa kuchoma matari.

Hata hivyo, upinzani nchini humo wanadai kuwa waliokufa katika tukio hilo wamefika watu 10 akiwamo mvulana mwenye umri wa miaka 14.

Kwa mujibu wa Reuters, polisi pia walivamia nyumba za waathirika.

Hata hivyo, mpaka sasa Serikali nchini humo haijatoa tamko lolote kuhusiana na shutuma hizo.