Watumia zebaki bila kujali athari watakazopata

Thursday February 13 2020

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Licha ya elimu inayotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhusu madhara yatokanayo na matumizi yasio sahihi ya zebaki, baadhi ya wachimbaji wadogo wameendelea kushika zebaki kwa mikono bila kutumia vifaa kinga.

Hayo yameshuhudiwa leo Alhamisi Februari 13, 2020 na waandishi wa habari  waliotembelea moja ya mgodi katika kijiji cha Nyakagwe wilayani Geita  kwa ajili ya kuona shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu.

Deus Amos, amesema hawavai vifaa kinga kwa kuwa wakivaa hawashiki vyema dhahabu.

Mmiliki wa mgodi huo Mohamed Mtalinge amesema licha ya kuwanunulia vifaa vya kujikinga lakini wengi hawavitumii na hata wakielezwa madhara hawaamini.

Mkurugenzi wa taasisi ya kuendeleza wachimbaji wadogo nchini (FADev),  Theonestina Mwasha  amesema taasisi hiyo imeanza kuwaelimisha wachimbaji wadogo kujua madhara ya zebaki pamoja na kuwajengea uwezo.

Mwasha amesema licha ya wachimbaji wadogo kuona zebaki ni kemikali nafuu kwao ,matumizi yasio sahihi yana madhara mbalimbali ikiwemo mtu kupoteza kumbukumbu ,kupata shida ya kutembea ,kutosikia vizuri, madhara kwenye figo na hata kifo.

Advertisement

Julai 3, 2019 Tanzania ilipitisha mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2024

 

Advertisement