Watumishi 127 wa EAC hatarini kupoteza ajira

Wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa jumuiya,Balozi Liberat Mfumukeko wakati akitoa hotuba ya mwaka mpya jijini Arusha jana.Picha na Filbert Rweyemamu

Arusha. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Liberat Mfumekeko, amewahakikishia wafanyakazi watakaondolewa baada ya mchakato wa kuifanyia jumuiya hiyo maboresho watapata haki zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za ajira za EAC.

Akizungumza na wafanyakazi hao makao makuu ya EAC jijini hapa pamoja na walio kwenye katika nchi wanachama kwa njia ya video (VC), Mfumukeko alisema Baraza la Mawaziri lishapitisha mabadiliko na kabla ya kutekelezwa Sekretarieti ilipeleka mapendekezo kwa baraza hilo. “Mwishoni mwa mwaka 2019, Baraza la Mawaziri la EAC lilipitisha ripoti ya maboresho ya jumuiya na utekelezaji wake, nafahamu kuna mambo ambayo wafanyakazi mmekua na wasiwasi nayo, napenda kuwahakikishia kila jambo linachukuliwa kwa umakini.”

“Tumewasilisha mapendekezo kwenye Baraza la Mawaziri, uamuzi wa mwisho bado haujachukuliwa hadi mapendekezo yetu yatakapopatiwa majibu. Kuweni na hakika wakati wa mchakato wa kuifanyia maboresho ya kitaasisi kupitia Mkataba wa EAC, taratibu za ajira zitazingatiwa,” alisema Mfumukeko.

Taarifa za ndani ya jumuiya hiyo zimedai kuwa wafanyakazi 127 kati ya 456 waliopo makao makuu ya jumuiya hiyo jijini hapa na kwenye taasisi katika nchi wanachama wataondolewa kufuatia mapendekezo ya Tume iliyoundwa ambayo ilijumuisha makamishna wa kazi kutoka nchi zote za EAC.

Upunguzaji wa wafanyakazi hao unaenda sambamba na kuondoa baadhi ya idara katika mfumo wa utendaji kazi kufuatia EAC kuelemewa na mzigo wa kuwalipa kutokana na jumuiya hiyo kuendeshwa kwa gharama za nchi wanachama ambazo zimekua hazichangii kwa wakati hivyo mishahara na shughuli nyingine kukwama.

“Hatujui hatma ya EAC itakavyokua kwa sababu kwa sasa kuna upungufu wa watumishi, kuna wakati ilifanyika uchambuzi wa kazi (Job Analyisis) ikaonekana idadi ya wafanyakazi ni ndogo ukilinganisha na kazi zilizopo na wafanyakazi wakipunguzwa, inaweza kusababisha magonjwa yanayotokana na wingi wa kazi,” alisema mmoja wa wafanyakazi.

Katika hotuba yake Balozi Mfumukeko alisema kampuni ya Ernest & Young ya Kenya imepewa jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna EAC inavyoweza ikaimarisha upatikanaji wa fedha za kuiendesha kutokana na utaratibu wa sasa wa nchi wanachama kusuasua na kukwamisha shughuli zilizopangwa na mishahara ya watumishi.

Kuhusu utendaji kazi wa jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka 20 iliyopita tangu kuanzishwa kwake, alisema licha ya mafanikio yaliyopatakana bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika nchi wanachama.