Watumishi tisa NSSF akiwamo bosi wa fedha wapandishwa kortini

Muktasari:

Wafanyakazi tisa wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) nchini Tanzania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji fedha zaidi ya Sh2 bilioni.

Dar es Salaam. Wafanyakazi tisa kutoka makao makuu  ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) nchini Tanzania akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Jamila Vullu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji fedha zaidi ya Sh2 bilioni
Mbali na Vullu wengine ni Mhadishi wa Hundi, Abdulrahaman Njozi, Meneja Uhakiki, Amiri Kapera, Mhasibu Mwandamizi, James Oigo, Mhasibu Mkuu, Hellen Peter, Mhasibu kitengo cha Madeni, Invonne Kimaro, Mhasibu dawati la Uchunguzi, Restiana Lukwaro, Kaimu Rasilimali watu, Tikyeba Alphonce na Mhasibu, Dominic Mbwete.
Akisoma hati ya mashtaka hayo leo Jumanne Oktoba 1, 2019 Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa shtaka wanaokabiliwa washtakiwa hao ni la uhujumu uchumi.
Simon alidai  kati ya Julai Mosi, 2016 na Septemba 4, 2017 maeneo Dar es Salaam washtakiwa hao pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani  walikula njama na kutakatisha fedha kiasi cha zaidi ya Sh2 bilioni wakiharibu kuonyesha hundi hizo halali zimetolewa na bodi ya wadhamini ya NSSF huku wakijua si kweli.
Katika shtaka la pili kati ya Julai Mosi, 2016 na Septemba 4, 2017 wakiwa katika ofisi za NSSF makao makuu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa Njozi na Kapera kwa nia ya kufanya udanganyifu walighushi jumla ya hundi 47 za benki ya CRDB ambazo ni akaunti namba 01J1028249500 ya bodi ya wadhamini ya NSSF.
Shtaka la tatu tarehe hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam washtakiwa wote wakiwa watumishi wa umma walioajiliwa waiiba zaidi ya Sh2 bilioni mali ya bodi ya wadhamini ya NSSF.
Simon alidai katika shtaka la nne tarehe hiyo hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu washtakiwa wote wakiwa watumishi wa umma waliisababishia hasara NSSF kiasi cha zaidi ya Sh2 bilioni kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Katika staka la tano tarehe hiyo hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu ya NSSF washtakiwa wote kwa pamoja walijihusisha na  miamala haramu ya zaidi ya Sh2 bilioni huku wakifahamu fedha hizo ni mazalio ya kosa tangulizi.
Simon alidai upelelezi bado haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine.
Hakimu Mhina alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo isipokuwa ni mahakama kuu pekee.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2014.